31.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 10, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji, yawaita wawekezaji zaidi kwenye madini

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Serikali imesema itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji ikiwemo kuboresha miundombinu ya umeme na usafirishaji na kutoa wito kwa kampuni za ndani na nje kuwekeza katika sekta ya madini hapa nchini.

Akizungumza leo Novemba 19,2024 wakati akifungua mkutano wa sita wa kimataifa wa wawekezaji katika sekta ya madini nchini, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema madini ni nguzo muhimu katika ukuaji wa uchumi nchini.

Amesema Serikali imeweka vivutio kwa kufanya marekebisho ya sheria na kanuni ili kuwawezesha wachimbaji na wafanyabiashara wa madini kufanya shughuli zao katika mazingira wezeshi.

“Nchi yetu ina sera nzuri, zimewekwa sheria na kanuni wezeshi kwa uwekezaji. Nchi yetu ina utulivu na amani ya kutosha lakini pia tuna utulivu wa kisiasa.

“Haya yote yanafanya mwekezaji ufanye maamuzi kuja kuwekeza hapa nchini, nisisitize umuhimu wa kuwekeza katika nchi yetu na masoko yanapatikana kwa sababu nchi yetu imekua kimkakati zaidi,” amesema Majaliwa.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, vivutio hivyo ni kupunguza ulipaji mrabaha kutoka asilimia 6 hadi nne, kupunguza ada ya ukaguzi kutoka asilimia moja hadi sifuri na kuondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa lengo la kuwafanya wachimbaji wadogo, wa kati na wakubwa kuongeza thamani na kuuza madini kwenye viwanda vya ndani.

Amesema pia bado nchi hainufaiki ipasavyo na uvunaji wa madini kwa sababu shughuli za uongezaji thamani zinafanyika nje ya nchi na kwamba Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi ili kuyaongezea thamani madini.

Aidha amewataka wachimbaji na wafanyabiashara wa madini kutekeleza takwa la kisheria la kuiuzia dhahabu Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ili kuwa na akiba ya kutosha kukabili changamoto ya uhaba wa fedha za kigeni.

Naye Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesisitiza kuwa hawatatoa leseni kubwa ya uchimbaji madini mpaka mwekezaji atakapothibitisha kwamba ataongeza thamani ili kuhakikisha madini yote yanaongezwa thamani kabla ya kusafirishwa nje ya nchi.

Waziri huyo amesema pia Sheria ya Uwezeshaji Wazawa (Local Content) imeleta manufaa makubwa katika sekta hiyo na hadi sasa zaidi ya Watanzania 16,700 wamepata ajira za moja kwa moja huku viongozi wakuu wa kampuni kwa kiasi kikubwa wakiwa pia ni Watanzania.

Aidha amesema leseni 2,648 zilizofutwa baada ya kushikiliwa na watu bila kuendelezwa sasa zitagawiwa kwa wachimbaji wadogo.

Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimba Madini Tanzania (Femata), Victor Tesha, ameishukuru Serikali kwa kutatua changamoto zao na kuiomba mashine za kuchoronga miamba ziongezwe ili kila wilaya iwe na mashine moja kuwarahishia wachimbaji na kuwa na takwimu za uhakika.

Mkutano huo wenye kaulimbiu isemayo ‘Uongezaji thamani madini kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii’ umelenga kujadili kwa pamoja mustakabali wa sekta ya madini, kushirikishana maarifa, ujuzi na kuangalia fursa mpya zinazojitokeza katika sekta hiyo inayokua kwa kasi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles