26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Kina Magoti waendelea kusota rumande

NA KULWA MZEE -DAR ES SALAAM

OFISA Programu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Tito Magoti na mwenzake wanaendelea kusota rumande huku wakilalamikia upelelezi kuchelewa kukamilika.

Kesi hiyo ilitajwa jana mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Janeth Mtega.

Wakili wa Serikali, Esther Martin alidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, lakini wamefuatilia kwa wapelelezi wamewaahidi kujitahidi wakamilishe.

Lakini Wakili wa utetezi, Jeremia Mtobesya alidai miezi sita imepita tangu washtakiwa wawe ndani, huku upande wa utetezi ukitoa kauli hizo kwa muda mrefu.

Alidai makosa yanayowakabili washtakiwa yangeweza kukamilishwa upelelezi kabla ya kukamatwa na kwamba ucheleweshwaji huo unaenda kinyume na kaulimbiu ya mahakama ya kuendesha kesi kwa haraka.

Aliiomba mahakama itoe karipio vinginevyo biashara hiyo haitaisha na wanatakiwa kujua washtakiwa wapo ndani na uhuru wao umechukuliwa.

Wakili Esther aliahidi kufanyia kazi suala hilo na Hakimu Mtega aliutaka upande wa Jamhuri kufuatilia kwa wapelelezi husika ili tarehe ijayo waje na hatua halisi waliyofikia.

Mshtakiwa mwingine kàtika kesi hiyo ni mtaalamu wa masuala ya Tehama (ICT), Theodory Giyan.

Kwa pamoja wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka matatu ikiwemo utakatishaji wa zaidi ya Sh milioni 17.

Mahakama iliahirisha kesi hiyo hadi Julai 8 kwa kutajwa.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka matatu ambayo ni kuendesha genge la uhalifu, kumiliki programu ya kompyuta kwa lengo la kutenda makosa ya jinai na kutakatisha zaidi ya Sh milioni 17.

Ilidaiwa kati ya Februari mosi hadi Desemba 17 mwaka jana katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam na ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa nia ovu wakiwa na wenzao ambao hawapo mahakamani, walishiriki genge la uhalifu na kujipatia Sh 17,354, 535.

Shtaka la pili ilidaiwa kuwa katika tarehe na maeneo hayo, washtakiwa hao wakiwa na wenzao ambao hawapo mahakamani, walitenda kosa la kumiliki programu ya kompyuta iliyotengenezwa mahususi katika kutenda makosa ya jinai.

Katika shtaka la tatu la utakatishaji fedha, ilidaiwa katika tarehe hizo jijini Dar es Salaam, washtakiwa hao wanadaiwa kujipatia Sh l 17,354, 535 wakati wakijua ni mazalia ya kosa la kuendesha genge la uhalifu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles