Na MAREGESI PAUL-DAR ES SALAAM
JUZI nilimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akiwapa maelekezo viongozi wa wizara, taasisi za umma na mikoa, kwamba wasiwatumie waandishi wa habari binafsi kuripoti habari za Serikali.
Kwa faida ya wale ambao hawakumsikia Waziri Mkuu Majaliwa, nawaambia kwamba, Waziri Mkuu alitoa maelekezo hayo alipokuwa jijini Mwanza, akifungua mkutano wa maofisa habari wa Serikali.
Ili kuhakikisha agizo lake linatekelezwa, Waziri Mkuu aliuagiza uongozi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, umpelekee majina ya viongozi au watendaji wa Serikali ambao wamekuwa na utaratibu wa kuwatumia waandishi wa habari binafsi na kuwaacha maofisa habari wa Serikali bila sababu za msingi.
Sipingani na Waziri Mkuu kwa sababu ni kweli kwamba, maofisa habari wa Serikali wanatakiwa kuripoti habari za Serikali kupitia vyombo vya habari ili ziwafikie wananchi kwa wakati unaotakiwa.
Pamoja na hali hiyo, nimelazimika kuandika maneno haya huku nikimwomba Waziri Mkuu asome makala haya kwa sababu naamini hawajui vizuri maofisa habari wa Serikali, japokuwa wamesomea masuala ya uandishi wa habari kupitia vyuo vinavyoheshimika nchini na duniani kwa ujumla wake.
Waziri Mkuu, napenda kukujulisha kwamba, baadhi ya maofisa habari walioko serikalini, uwezo wao wa kuandika habari na makala zinazoihusu Serikali na nyinginezo ni mdogo kiasi kwamba hawana hata uthubutu wa kufanya hivyo kupitia vyombo vya habari.
Huko serikalini ambako Waziri Mkuu Majaliwa unataka maofisa habari waandike habari za Serikali, ndiko kuna maofisa habari wasiokuwa karibu na vyombo vya habari.
Nasema hivyo kwa sababu idadi kubwa ya maofisa habari wa Serikali unaotaka waandike habari za Serikali, hawana ukaribu wowote na vyombo vya habari bila kujali chombo hicho kinamilikiwa na Serikali au chombo hicho kinamilikiwa na watu binafsi au taasisi binafsi.
Maofisa habari wa Serikali wamejifungia huko serikalini, hawajui ofisi za vyombo vya habari ziko wapi, hawajui wahariri wa vyombo vya habari ni akina nani, hali kadhalika hawajui habari zinachakatwaje japokuwa nao ni waandishi wa habari wenzetu.
Wakati baadhi ya maofisa habari hao wakiishi kivyao vyao katika ulimwengu wa habari, litakuwa ni jambo gumu sana kwao kufanyakazi na watu wasiowajua katika vyombo vya habari na itakuwa vigumu pia kwa wahariri kufanyakazi na watu wasiowajua hata kama ni maofisa habari serikalini.
Waziri Mkuu, ukitaka kuamini ninachokwambia, fanya ziara ya kushtukiza katika wizara au ofisi yoyoye ya umma na waulize maofisa habari wa ofisi hiyo, kama wanajua chochote kuhusu vyombo vya habari vya Tanzania ambavyo wanatakiwa kufanya navyo kazi.
Utakapokuwa unawauliza hayo, waulize ofisi za Gazeti la Mtanzania ziko wapi, waulize ofisi za habari za magazeti ya Nipashe, Mwananchi, Tanzania Daima, Majira, Dimba, Rai, Bingwa, Mwanaspoti, Habari Leo, Uhuru na Mzalendo ziko wapi ili uone kama wanaelewa zilipo.
Waziri Mkuu, kwa kuwa vyombo vya habari viko vingi, unaweza pia kuwauliza mahali zilipo ofisi za ITV, Star TV, Azam Tv, TBC, Capital TV, Kwanza TV, Channel Ten na nyinginezo nchini.
Waziri Mkuu, kama utakuwa na muda wa kutosha, basi naomba uwaulize kama wamewahi kuandika habari yoyote ikatoka gazetini au kwenye chombo chochote cha habari kwa sababu nina hakika baadhi ya maofisa habari wa Serikali, hawajawahi kuripoti habari yoyote katika vyombo vya habari ingawa ni maofisa habari wa ofisi wanazozifanyia kazi.
Waziri Mkuu, nakuomba uwaulize maswali hayo kwa sababu naamini maofisa wengi wa Serikali hawajawahi kutembelea vyombo vya habari na hawajui vyombo hivyo viko wapi, hawajui vinafanyaje kazi na hawajui vinaongozwa na akina nani, japokuwa sasa umewaagiza wafanye kazi ya kuandika habari kupitia vyombo vya habari.
Pamoja na hayo, napenda kukwambia jambo moja kubwa ambalo huenda baadhi ya watu hawataki kukwambia kutokana na sababu wanazozijua wao.
Katika eneo hilo, napenda kukwambia kwamba, idadi kubwa ya maofisa habari wa Serikali, hawajui kupiga picha kwa ajili ya televisheni na picha za mnato, picha za habari kwa njia ya dijitali na wengi wao hawajui kuandika habari kwa ajili ya magazetini achilia mbali habari za kwenye televisheni na redio ambako pia wanatakiwa kuripoti kama ulivyoelekeza.
Nasema hawajui kupiga picha na kuandika habari hizo kwa sababu idadi kubwa ya maofisa hao, wameingia serikalini wakitokea vyuoni na hawajawahi kufanya kazi katika chombo chochote cha habari ambako ndiko habari zinakotafutwa na kuandaliwa, kuchakatwa kwa ajili ya wananchi.
Unaweza ukajiuliza ni kwanini maofisa habari hao hawajui kuandika habari hizo wakati wana ufaulu mzuri wa GPA za kuanzia 3.5 na kuendelea, lakini ukweli ni kwamba, maofisa habari hao hawajui kuandika habari kwa sababu vyuo vyetu vingi havina vyombo vya habari vya kujifunzia.
Kwa maana hiyo, mwanafunzi anapotoka chuoni na GP yake nzuri kisha akaomba kazi ya uofisa habari serikalini, hatakuwa na uwezo mpana wa kuandika habari ili itakapofika kwa mhariri isimpe shida.
Pamoja na hayo, Waziri Mkuu napenda kukuhakikishia kwamba, kati ya ofisi za umma zenye bahati ya kupata waandishi wa habari wenye uwezo wa kuandika habari zisizoumiza vichwa vya wahariri, ni ofisi yako.
Hapo ofisini kwako una mwandishi wa habari mkongwe na aliyewahi kuishi na kufanyakazi katika vyombo vya habari kabla hajaingia serikalini, Iren Bwire.
Iren ambaye ni mkongwe katika tasnia ya habari nchini, anajua kuandika habari na naamini hakuna chombo chochote cha habari nchini, kisichokuwa na mwandishi ambaye hamfahamu.
Sambamba na huyo, ofisini kwako unaye mwandishi wa habari wa siku nyingi ambaye pia ni mwanafunzi mwenzangu wa Shahada za uzamili katika chuo kikuu kimoja nchini, Khadija Mussa.
Khadija kabla hajafanya kazi serikalini, alikuwa akiishi na kufanya kazi katika chombo cha habari kwa miaka mingi.
Kutokana na hali hiyo, Khadija ana uwezo usiokuwa na shaka, kwani anajua kuandika habari zisizokuwa na matege kama ilivyo kwa maofisa habari wengine wa Serikali.
Kwa hiyo, wewe Waziri Mkuu bahati uliyonayo ya kuwa na maofisa habari ambao ni waandishi wa habari waliowahi kufanya kazi katika vyombo vya habari, mawaziri na maofisa wengine wa Serikali, hawana bahati hiyo.
Badala yake, mawaziri na maofisa wengine wa Serikali, wana maofisa habari wenye vyeti vizuri, lakini hawajawahi kukaa chumba chochote cha habari kwa ajili ya kuandika habari ambazo unataka wazipeleke katika vyombo vya habari badala ya waandishi wa habari binafsi.
Kwa maana hiyo, kama maofisa hao hawatataka kujifunza kuandika habari na badala yake wakaendelea kuamini GPA za kwenye vyeti walivyonavyo, habari unazotaka waziandike hazitatoka kwa kiwango unachotarajia kwa sababu wahariri siku zote wanataka habari zisizowaumiza vichwa wakati wa kuhariri.
Pamoja na maelezo hayo niliyoyasema, Waziri Mkuu, nakushauri utoe maelekezo kwa maofisa habari serikalini, watembelee vyombo vya habari, wafahamiane na wenzao walioko huko na pia wawe na utaratibu wa kuandika habari maana baadhi yao hawajui hata kuandaa press release.
Binafsi, naamini kama wataanza kutembelea vyombo hivyo vya habari, wataanza kujenga uhusiano mzuri na waandishi wa habari wengine pamoja na wahariri wa vyombo hivyo vya habari kiasi kwamba itakuwa rahisi pande hizo mbili kufanya kazi kwa ushirikiano kwa kuwa zitakuwa zinafahamiana.
Utakapokuwa unawaelekeza hayo, waambie wao ni waandishi wa habari sawa na waandishi wa habari walioko katika vyombo vya habari japokuwa wao wako serikalini ambako ndiko kunapatikana habari nyingi kuliko sehemu nyingine yoyote.