29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Wazazi wasikilizeni watoto kabla ya kuwaadhibu

Na MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

TABIA za wazazi mara nyingi zinaweza kuchongwa na mazingira ya kimalezi. Mambo uliyoshuhudia yakitokea wakati ukikua, au wakati mwingine uliyoona yakifanywa na watu muhimu kwenye maisha yako, yana nafasi kubwa ya kutengeneza hulka fulani zinazoongoza namna unavyowalea watoto wako.

Hulka hizi huathiri uamuzi wa wazazi bila wenyewe kuelewa kinachotokea.

Fikiria mzazi aliyelelewa na wazazi waliokuwa na misuguano isiyoisha. Mzazi aliyeshuhudia wazazi wake wakipigana, wakitukanana na pengine kutengana. Matukio kama haya yanaweza kuathiri mtazamo wa mzazi huyu si tu kuhusu ndoa lakini pia kuhusu malezi.

Mfano namna ambavyo unawaadhibu watoto wako na unavyozungumza nao, kwa kiasi kikubwa ni matokeo ya mkusanyiko wa alama ulizoachiwa na wazazi wako. Alama hizi hutengeneza sauti fulani inayokunong’oneza na kuwa sehemu ya utambulisho wako.

Habari njema ni kwamba bila kujali ulilelewa katika mazingira yaliyokuumiza kwa kiwango gani, bila kujali ulionewa kwa kiasi gani, ukiwa mzazi, unazo nguvu za kuchagua kuwa mzazi bora. Uwezo huo upo katika mamlaka yako mwenyewe. Ili kuupata uwezo huo, hatua ya kwanza ni kukubali kuwa kuna vitu visivyo sahihi, unaweza kuwa ulivirithi lakini vinaathiri namna unavyolea watoto wako. Usiendelee kuchukulia kawaida, unapogundua una tabia ya kupiga kelele unapowaelekeza watoto wako. Kelele si tabia ya kawaida na hakuna mtu anayezaliwa akiwa mpiga kelele bali mazingira ya kimalezi humfanya awe hivyo. Kuendelea kuchukulia kelele kuwa jambo la kawaida, ni kuendeleza mnyonyoro wa tabia hiyo kwa watoto wako.

Badala ya kupiga kelele, unaweza kujifunza kumsikiliza mtoto kabla hujadai afanye unavyotaka. Wakati mwingine mtoto hakusikilizi na unalazimika kufoka kwa sababu hujaweza kumfanya ajisikie kusikilizwa. Ukimsikiliza, unaweza kuona mabadiliko. Badala ya kuwa mwepesi kuchapa, kutukana na kukosoa muda mwingi, unaweza kujifunza kujenga uhusiano mzuri na mwanao utakaokusaidia kumrekebisha bila kulazimika kutumia nguvu. Badala kufanya uamuzi ukiwa na hasira, unaweza kubadilika na kuanza kushughulikia tatizo baada ya kutuliza hasira zako.

Fanya uamuzi sasa, lea watoto wako katika misingi iliyonyooka bila kutafakari yaliyokutokea huko nyuma.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles