PRAGUE, CZECH
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Czech, Andrej Babis alijikuta akizomewa wakati akitoa hotuba katika kumbukumbu ya miaka 50 ya uvamizi ulioongozwa na uliokuwa Umoja wa Kisoshalisti wa Kisovieti (USSR) katika iliyokuwa Czechoslovakia.
Siku kama ya juzi Agosti 21, 1968 vifaru vya USSR viliingia mjini Prague kuzima mageuzi ya kidemokrasia ya Serikali ya Kikomunisti ya Czechoslovakia, na kuzusha umwagaji damu katika hatua ya kuikalia nchi hiyo.
Kumbukumbu hiyo ilifanyika kwa sherehe, maonesho na filamu juu ya vuguvugu la mapinduzi ya Prague pamoja na ukandamizaji wake wa kikatili.
Na imekuja katika wakati, ambao kuna ushawishi unaorejea tena katika chama cha kikomunisti, ambacho kwa muda mrefu kiliwekwa kando katika siasa za taifa hilo.
Babis, ambaye aliwahi kuwa mwanachama wa chama hicho cha Kikomunisti cha Czechoslovakia, alikuwa akizungumza katika kumbukumbu hiyo wakati maneno yake yalipomezwa na kelele za kumzomea; ‘aibu’, ‘aibu’, aibu’.
“Watu hawakutaka tena udikteta wa aina ya Kisovieti. Walitaka tu kuishi maisha ya kawaida ya jamii huru. Uvamizi wa majeshi ya mkataba wa Warsaw ulizuia hatua za mageuzi na ubinafsishaji, alisema huku akizomewa kwa kile kinachohesabiwa kuwa yu mnafiki.
Mwasisi huyo wa Chama cha ANO, ambaye amekuwa katika wadhifa wa uwaziri mkuu tangu mwaka jana amekuwa akikabiliwa na ukosoaji mkubwa unaohusiana na uanachama wake wa zamani katika chama cha kikomunisti.
Akizungumza katika kumbukumbu hiyo katika jengo la Redio ya Czech, eneo, ambalo machafuko makubwa yalitokea wakati wa uvamizi wa mwaka 1968, Babis alitoa heshima zake kwa wale waliofariki.
Katika tukio hilo linalokumbukwa, miezi miezi michache ya kuchukua madaraka kama kiongozi wa chama cha Kikomonisti cha iliyokuwa Czechoslovakia mwanzoni mwa 1968, Alexander Dubcek alifuta ubaguzi wa kisiasa, na kujaribu kuleta mageuzi ya kiuchumi hatua ambayo ilionekana kwenda kinyume na USSR.
Hivyo vikosi vya USSR ya zamani, Poland, Hungary na Bulgaria viliingia katika mji mkuu wa Czechoslovakia -Prague usiku wa Agosti 20-21 mwaka huo na kufanya ukandamizaji wa kikatili katika kile walichokiona ni kitisho kikubwa kwa ushawishi wa kisiasa wa Urusi.
Wanahistoria wanasema raia 137 waliuawa katika ukandamizaji huo kati ya Agosti na Desemba 1968.