WAZIRI MKUU AZOMEWA AKIHUTUBIA KUMBUKUMBU CZECH

0
699

 

PRAGUE, CZECH


WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Czech, Andrej Babis alijikuta akizomewa wakati akitoa hotuba katika kumbukumbu ya miaka 50 ya uvamizi ulioongozwa na uliokuwa Umoja wa Kisoshalisti wa Kisovieti (USSR) katika iliyokuwa Czechoslovakia.

Siku kama ya juzi Agosti 21, 1968 vifaru  vya USSR  viliingia  mjini  Prague  kuzima mageuzi ya kidemokrasia ya Serikali ya Kikomunisti  ya Czechoslovakia, na kuzusha umwagaji damu katika hatua ya  kuikalia nchi hiyo.

Kumbukumbu hiyo ilifanyika  kwa  sherehe, maonesho na  filamu juu  ya  vuguvugu  la mapinduzi ya Prague pamoja na ukandamizaji  wake  wa kikatili.

Na imekuja katika  wakati, ambao kuna ushawishi  unaorejea tena katika chama cha kikomunisti, ambacho kwa muda mrefu kiliwekwa  kando katika  siasa  za  taifa  hilo.

Babis, ambaye  aliwahi  kuwa  mwanachama  wa chama hicho cha Kikomunisti cha Czechoslovakia, alikuwa  akizungumza katika kumbukumbu  hiyo  wakati  maneno  yake  yalipomezwa na kelele  za kumzomea; ‘aibu’, ‘aibu’, aibu’.

“Watu hawakutaka tena udikteta wa aina ya Kisovieti. Walitaka tu  kuishi maisha ya kawaida ya jamii  huru. Uvamizi wa  majeshi ya  mkataba  wa  Warsaw ulizuia hatua  za mageuzi  na ubinafsishaji, alisema huku akizomewa kwa kile kinachohesabiwa kuwa yu mnafiki.

Mwasisi huyo wa Chama cha ANO, ambaye amekuwa katika wadhifa wa uwaziri mkuu tangu mwaka jana amekuwa akikabiliwa na ukosoaji  mkubwa unaohusiana na uanachama wake wa zamani katika chama cha kikomunisti.

Akizungumza  katika kumbukumbu  hiyo katika  jengo  la Redio ya  Czech, eneo, ambalo machafuko  makubwa  yalitokea  wakati wa  uvamizi wa mwaka 1968, Babis alitoa  heshima  zake kwa wale  waliofariki.

Katika tukio hilo linalokumbukwa, miezi miezi michache ya kuchukua madaraka  kama kiongozi wa chama cha Kikomonisti cha iliyokuwa Czechoslovakia mwanzoni mwa 1968, Alexander Dubcek alifuta ubaguzi wa kisiasa, na kujaribu kuleta mageuzi ya kiuchumi hatua ambayo ilionekana kwenda kinyume na USSR.

Hivyo vikosi vya USSR ya zamani, Poland, Hungary na Bulgaria viliingia katika mji mkuu wa Czechoslovakia -Prague usiku wa Agosti 20-21 mwaka huo na kufanya ukandamizaji wa kikatili katika kile walichokiona ni kitisho kikubwa kwa ushawishi wa kisiasa wa Urusi.

Wanahistoria wanasema raia 137 waliuawa katika ukandamizaji huo kati ya Agosti na Desemba 1968.

 

 

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here