28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, December 1, 2024

Contact us: [email protected]

AFRIKA YAANZA MKAKATI WA KUONDOA VIKWAZO VYA BIASHARA

Na ELIYA MBONEA, ARUSHA


NCHI za Bara la Afrika, zimeanza mkakati wa ushirikiano wa kibiashara kwa kuondoa vikwazo vya kibiashara ikiwamo ushuru wa forodha   ili kuunganisha soko la Afrika kuwa   moja  katika biashara ya bidhaa na huduma

Hatua hiyo imekuja ikiwa ni utekelezaji wa mawazo ya waasisi wa Bara la Afrika waliokuwa na ndoto ya kuliunganisha bara hilo kuwa moja katika nyaja za kibiashara na masoko.

Akizungumza juzi, wakayi wa mkutano huo, Kaimu Mkurugenzi  wa Idara ya Biashara, Uwekezaji na Sekta za Uzalishaji Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bernard Haule,alisema mkutano huo ni sehemu ya majadiliano katika ngazi ya wataalamu kuweza kuweka mikataba ya ushirikiano  katika hatua nzuri.

Alisema takwimu za biashara kwa nchi za Afrika, zinaonyesha asilimia 20 pekee  ya nchi hizo  zinafanyabiashara ya ndani, kiasi ambacho ni kidogo ikilinganishwa na nchi za Ulaya, zinazofanya biashara ya ndani kwa asilimia 50.

‘’Nchi za Afrika zinafanyabiashara kwa asilimia 20, huku asilimia 80 zinauza  mataifa ya nje na hiyo inatokana na changamoto ya vikwazo vya kibiashara vilivyopo katika nchi za Afrika,’’alisema

Alisema kwa kutambua hilo nchi hizo zimeamua  kuondoa  vikwanzo vya kibiashara ikiwamo kupunguza ushuru wa forodha ama kuondoa kabisa ili ziweze kuuziana bidhaa kwa unafuu zaidi jambo ambalo litawezesha kukuza uchumi bara la Afrika,tofauti na hali iliyopo kwa sasa.

‘’Mkataba huu utakapoanza  kufanya kazi biashara zitaongezeka kutoka tulipo sasa walau ifikie asilimia 50 ya biashara kama yalivyo mabara ya Ulaya ambapo biashara nyingi inafanyika ndani kwa ndani kuliko zinazouzwa nje, ndio hatua tunayoitaka kwa sasa,” alisema Haule.

Akizungumzia athari ya  kuondoa ushuru wa forodha kwa nchi za afrika zinazojiendesha kwa kutegemea kodi na ushuru mbalimbali alifafanua kuwa jambo hilo litachochea ongezeko la biashara za ndani na hivyo  mapato ya serikali yatapata kutokana na uwekezaji kuwa mkubwa.

Kwa upande wake, mshauri wa biashara na viwanda kutoka shirika la CFTA  UNIT,Prudence Sebahizi alisema kukutana kwa nchi  wanachama wa AU,kutasaidia kuimarisha uhusiano wa kibiashara kutokana na makubaliano ya kibiashara  yaliyosainiwa nchini Rwanda.

Naye Kaimu Mkurugenzi Msaidizi  Wizara ya Viwanda na Uwekezaji,Ombeni Mwasha alisema, mkutano huo umeandaliwa na Kamisheni ya Umoja wa Ulaya (AU),ukiwa na lengo la kuunda eneo huru la biashara kwa nchi hizo na kuiwashirikisha wataalamu wa masuala ya kibiashara na wanasheria  kutoka nchi 54.

Alisema mkataba wa kuunda  mpango huru wa kibiashara ulisainiwa Machi 21, mwaka huu, Rwanda kwa lengo kuimarisha uhusiano wa kibiashara kwa nchi hizo ili kukamilisha ndoto za wakuu wa nchi za Afrika waliokuwa na malengo ya kuifanya kuwa moja.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles