NA FRANCIS GODWIN,IRINGA
WAZIIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo ametoa maagizo mawili kwa Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela.
Miongoni mwa maagizo hayo, ni kuwakamata na kuwachukulia hatua kali wananchi wanaochafua mazingira na kufikishia agizo kwa Wakala wa Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) kutengeneza barabara ya kwenda Shule ya Sekondari Kihesa.
Akizungumza na wanafunzi na walimu wa Shule ya Sekondari Kihesa jana, Waziri Jafo alisema shule hiyo imekuwa ya kwanza nchini kwa kufanya vizuri katika ukusanyaji wa chupa za plasitiki ambazo zimekuwa zikitupwa ovyo mitaani na wananchi wasiojali mazingira .
Alisema kwa kuweka mkakati kabambe wa kuwawajibisha watu wanaochafua mazingira, utasaidia miji kuwa katika hali ya usafi.
Alisema wajibu wa kutunza mazingira, ni wa kila mmoja na ndio maana Rais Dk. John Magufuli alianzisha usafi kila mwisho wa mwezi nchi nzima.
“Lazima kila mmoja wetu kuunga mkono jitihada mbalimbali zinazofanywa na rais wetu Dk. John Magufuli katika maendeleo…hata suala hili la usafi ni wajibu wetu sote kuweka mazingira katika hali ya usafi,asitokee mwingine anafanya usafi na mwingi anachafua,” alisema waziri Jafo
Alimtaka Kasesela kufikisha salamu zake kwa Meneja wa TARURA Mkoa wa Iringa kuhakikisha anatengeneza barabara ya kutoka Semtema hadi Kihesa ili iweze kupitika wakati wote tofauti na ilivyo sasa.
“Mkuu wa wilaya nakuagiza kawaambie TARURA,waziri nimeagiza barabara hii ifanyiwe ukarabati hata kama si kwa kiwango cha lami,itengenezwe kwa kiwango cha changarawe na iweze kupitika vizuri “
Wakati huo huo,Waziri Jafo aliwataka wananchi kushiriki katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na vijiji ambao unataraji kufanyika mapema mwezi ujao .
” Mwaka 2019, ni mwaka wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa, nawapongeza Watanzania wamejitokeza kwa wingi kujiandikisha kwa mara ya kwanza tumevunja rekodi, maana lengo letu lilikuwa tuandikishe watu milioni 22.9 waliojiandikisha ni milioni 19.6 sawa na asilimia 86,”alisema.
MWISHO