ASHA BANI-DAR ES SALAAM
WAUAJI wilayani Rufiji Mkoa wa Pwani ‘wamembipu’ Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro, kwa kuua mtu mwingine usiku wa kuamkia jana katika Kitongoji cha Kazamoyo Kijiji cha Ikwiriri Kaskazini wilayani humo.
Wauaji hao walivamia kijijini hapo na kumpiga risasi shingoni, Erick Mwarabu (38) ambaye ni fundi rangi.
Kwa mujibu wa mtoa taarifa, Mwarabu akiwa nyumbani kwake saa 8.00 usiku juzi, wauaji hao walifika na kumpiga risasi shingoni ambayo ilitokea kichwani upande wa kulia kati ya jicho na sikio na akafariki dunia papo hapo.
Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Juma Njwayo, aliithibitishia MTANZANIA kwa simu kwamba tukio hilo la mauaji lilitokea usiku wa kuamkia jana.
Alisema tayari mwili wa marehemu umekwisha kufanyiwa uchunguzi na kukabidhiwa kwa ndugu zake kwa mazishi.
Kifo cha Mwarabu kinafanya idadi ya watu waliouawa hadi sasa katika wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji mkoani Pwani kufikia 30.
Kutokana na vitendo hivyo vya mauaji, hivi karibuni IGP Sirro, alitangaza mkakati wake ikiwamo jinsi ya kukomesha mauaji katika maeneo hayo.
IGP Sirro aliapa kupambana na wauaji hao huku akiahidi donge nono la Sh milioni 10 kwa yeyote atakayetoa taarifa za kuwezesha kukamatwa wauaji hao.
Alisema polisi wanaendelea na operesheni mbalimbali kuhakikisha vitendo hivyo haviendelei na kwamba lazima watafanikiwa kubaini mzizi wa mauaji hayo.
Mei 21 mwaka huu, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, alitembelea eneo hilo na kuteta na askari wa operesheni maalumu ya kuwasaka wauaji wilayani Kibiti.
Alisema mauaji hayo sasa yametosha akisisitiza Serikali haitakuwa tayari kuona vitendo hivyo vikiendelea kama ilivyo Somalia.
Ziara hiyo ya ghafla ya Waziri Nchemba ilitokana na mauaji ya mara kwa mara ya raia ambayo yamekuwa yakifanywa na watu wasiojulikana.
Akizungumza baada ya kuwatembelea polisi katika kambi maalumu ya operesheni ya kusaka wahalifu katika Kata ya Bungu, alisema Serikali imejipanga kukomesha hali hiyo kwa sababu kufuga wauaji na wahalifu kuna gharama.
“Tunaendelea kufuatilia kazi mnayoendelea kufanya, tuendelee kusonga mbele. Nikiziangalia takwimu na mwenendo, nazidi kupata maswali na naendelea kuona kuwa kuna kamchezo kanachezwa.
“Mauaji haya waliyoyafanya inatosha. Lazima tuwatie nguvuni, hatuwezi kuruhusu jambo hili likaendelea na kamchezo haka kakaendelea.
“Anayefanya mauaji haya, anayeshirikiana na anayeshangilia hiki kinachofanyika wote tunawaweka katika kundi moja. Kufuga wauaji na wahalifu kuna gharama,”alisema.
Nchemba aliwataka polisi hao kukaa kimkamkati kuwakamata wauaji hao.
Alisema ni muhimu polisi waondokane na dhana kwamba wametokomea kusikojulika bali wawakamate.