25.7 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

WATAALAMU SEKTA YA AFYA KUPEWA LESENI

profesa-muhammad-kambiNA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

WATAALAMU wa kada mbalimbali za sekta ya afya, sasa wataanza kusajiliwa na kupewa leseni zitakazowatambulisha na zitakuwa na masharti maalumu.

Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Muhammad Kambi, alisema hayo Dar es Salaam jana, alipofungua mkutano wa mwaka wa Chama cha Wafiziotherapia (APTA).

Alisema Serikali imeanza mchakato wa kuipitia upya Sheria ya Madaktari wa Tanganyika, ambayo itaongezwa sharti hilo pamoja na kuundwa kwa bodi maalumu itakayosimamia maadili ya watumishi hao.

“Sekta ya afya kama zilivyo sekta nyingine nayo imekua. Wakati ilipoanzishwa, sheria hii ilikuwa ikiwatambua madaktari na wauguzi pekee.

“Lakini hivi sasa kuna taaluma nyingi ndani ya hii fani, kwa mfano ninyi wataalamu wa fiziotherapia. Mpo lakini sheria haiwatambui, kwa maana hiyo inakuwa vigumu hata kuwafuatilia. Ndiyo msingi wa kuipitia upya sheria hii.

“Katika sheria mpya itakayoboreshwa, kila mtumishi atatakiwa kukata leseni. Kila mtumishi atatakiwa kujiendeleza elimu, kuongeza ujuzi ili aendane na wakati uliopo kwa sababu mambo yanabadilika, kile ulichosoma jana unahitaji kujifunza zaidi,” alisema.

Profesa Kambi alisema tayari maboresho ya sheria hiyo yameshawasilishwa katika Kamati ya Baraza la Mawaziri ya Katiba na Sheria na imeshapitiwa.

“Baadaye italetwa kwenu wadau mpate fursa ya kutoa maoni kabla ya kupelekwa bungeni kujadiliwa, lakini pamoja na hayo, nawasihi wataalamu wote mfanye kazi kwa kuzingatia maadili,” alisema.

Awali, Rais wa APTA, Remla Shirima, alisema moja ya changamoto zinazokabili fani hiyo ni uhaba wa wataalamu.

“Tanzania nzima kuna fiziotherapia 350 tu, ni idadi ndogo mno, tuna uhaba pia wa vifaa kwa ajili ya kuwasaidia wagonjwa kufanya mazoezi yao.

“Lakini pia kwa sababu hakuna sheria inayosimamia wataalamu, tiba ya mazoezi imekuwa ikitolewa holela na mtu yeyote anayejisikia kufanya hivyo, hii ni hatari,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles