26.6 C
Dar es Salaam
Sunday, April 14, 2024

Contact us: [email protected]

WAKILI APINGA KUSIKILIZWA MAOMBI ‘SAMAKI WA MAGUFULI’

samaki-wa-magufuliNa Kulwa Mzee-Dar es Salaam

WAKILI wa Serikali Mkuu, Timon Vitalis, amedai Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam haiwezi kusikiliza maombi ya ‘Wachina wa Masamaki wa Magufuli ‘ya kutaka kurejeshewa meli yao iliyozama na samaki kwa sababu amri ya kurejeshewa ilitolewa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Meli hiyo iliyozama na samaki tani 296.3 waliotaifishwa na Serikali pamoja na vitu vyote ina thamani ya zaidi ya Sh bilioni saba.

Vitalis aliwasilisha hoja za kupinga maombi hayo kusikilizwa jana katika mahakama hiyo mbele ya Jaji Ama-Isario Munisi wakati maombi yalipotakiwa kuanza kusikilizwa.

Upande huo wa Jamhuri ulidai mwombaji katika maombi hayo ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Tawariq, Said Mohammed, hana sifa ya kukabidhiwa mali hiyo.

“Mheshimiwa Jaji, upande wa Jamhuri tunaomba mahakama itupilie mbali maombi ya kutaka kurejeshwa meli ya Tawariq 1 na zaidi ya Sh bilioni mbili  za tani 296.3 za samaki.

Maombi hayo yalitokana na kesi  iliyokuwa inawakabili    Nahodha wa Meli, Hsu Chin Tai na Wakala wa Meli ya Tawaliq 1, Zhao Hanquing.

Watu hao walikuwa  wakikabiliwa na mashtaka ya uvuvi haramu katika ukanda wa Uchumi wa Bahari ya Tanzania.

Washtakiwa hao walikamatwa mwaka 2009 na boti ya askari wa doria wa   Tanzania, Afrika Kusini, Botswana.  Leseni waliyokuwa nayo ilikuwa imemaliza muda wake Desemba mosi, mwaka 2008.

Wakili Vitals alidai   maombi hayo hayastahili kusikilizwa na Mahakama Kuu kwa sababu amri ya kurejeshwa mali hizo ilitolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwamba washtakiwa wakabidhiwe mali zote walizokamatwa nazo ikiwamo meli hiyo.

Alidai haiwezekani maombi hayo yapelekwe Mahakama Kuu  kwa sababu Mahakama ya Kisutu ilishaamuru, mali akabidhiwe mshtakiwa wa kwanza aliyekuwa kapteni wa meli hiyo.

Vitalis alidai Mahakama ya Rufaa ilishafuta mwenendo wa kesi ya msingi wa Mahakama Kuu.

Alidai  kwa sababu hiyo maombi hayo ni batili hayawezi kusikilizwa na kutolewa amri mbili katika mahakama mbili zinazohusu kitu kimoja.

Wakili  alidai mahakama hiyo haiwezi kuamuru  mkurugenzi huyo kurejeshewa mali hizo wanazodaiwa kwa kuwa siyo kampuni yake.

Jamhuri ilidai kama wadai wana hoja waziwasilishe katika mahakama iliyotoa amri hiyo ambayo ni Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Mdai katika maombi hayo ni mwajiri wa wachina hao, Said Mohammed, anawakilishwa na  Mawakili Kapteni Ibrahim Bendera na John Mapinduzi.

Mawakili hao walifungua kesi hiyo kwa hati ya dharura dhidi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), wakidai Meli ya Tawariq 1yenye thamani ya Dola za Marekani 2,300,000 na   Sh 2,074,249,000 ambazo ni gharama za samaki zilizofanyiwa uthamini Oktoba mosi, 2009.

Meli hiyo ilifanyiwa uthamini mwaka 2008 na kuonyesha kwamba thamani yake ni Dola 2,300,000.  Ripoti hiyo ilitolewa na Kampuni ya Cambodia Shipping Services Ltd.

Akijibu hoja za Jamhuri, Kapten Bendera alidai kuwa waliwasilisha maombi hayo mahakamani hapo kwa sababu Mahakama ya Kisutu ilikataa kurejesha mali hizo kwa mshtakiwa wa kwanza.

Kapteni Bendera alidai waliwasilisha maombi hayo Mahakama Kuu kwa sababu vielelezo vilitolewa katika mahakama hiyo wakati wa usikilizwaji wa kesi ya msingi.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Jaji Munisi alisema mahakama yake itatoa uamuzi Desemba 7 mwaka huu.

Agosti mwaka 2014 Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliwaachia huru Wachina wa ‘Samaki wa Magufuli’ na kuamuru Jamhuri iwarejeshee vitu vyao, ikiwamo meli ya Tawariq 1.

Wachina hao waliachiwa kwa mara ya pili, mara ya kwanza waliachiwa na Mahakama ya Rufaa Machi 28, 2014 , lakini walikamatwa tena na kushtakiwa upya kwa mashtaka hayo hayo yaliyofutwa.

Septemba mosi, mwaka 2014 , wadai waliwasilisha barua  ya maombi hayo mbele ya Msajili wa Mahakama hiyo.

Katika barua hiyo, wanaomba mahakama iwarejeshee vielelezo vilivyotolewa mahakamani wakati kesi namba 38 ya mwaka 2009 mbele ya Jaji Radhia Sheikh iliposikilizwa.

Barua hiyo ilivitaja vielelezo hivyo kuwa ni meli ya uvuvi Tawariq 1 pamoja na Sh 2, 074,249,000 za tani 296.3 za samaki walizokutwa nazo raia hao ambavyo vilitolewa Oktoba mosi, mwaka 2009 mbele ya Jaji Sheikh.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles