Na Allan Vicent, Tabora
WAKUU wa Vyuo vya Ualimu Kanda ya Magharibi, wamewataka kuimarisha michezo katika vyuo vyao ili kukuza vipaji na kuandaa viongozi watakaosimamia sekta hiyo katika maeneo ya kazi wanapohitimu masomo.
Ushauri huo umetolewa jana na Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Dk.Yahaya Nawanda wakati wa ufunguzi wa mashindano ya Kanda ya Magharibi ya Umoja wa Michezo na Sanaa katika Vyuo vya Ualimu Tanzania (UMISAVUTA) katika viwanja vya Chuo cha Ualimu Tabora.
Amesema michezo huimarisha afya, kutoa ajira na kuleta burudani miongoni mwa jamii, hivyo kama itahamamsishwa na kuimarishwa ipasavyo vyuoni Taifa litapata wachezaji na viongozi mahiri watakaosimamia sekta hiyo.
‘Vyuo vya ualimu vina nafasi kubwa ya kukuza vipaji vya michezo kwa wanachuo ikiwamo kuandaa walimu na makocha wa michezo mbalimbali wanapomaliza masomo yao,” amesema.
Aidha amewataka kutumia mashindano hayo ya siku tano kuchagua timu ambazo zitapeperusha vyema bendera ya Kanda hiyo katika mashindano ya UMISAVUTA Taifa yanayotarajiwa kufanyika mkoani Mtwara kuanzia Novemba 29 hadi Desemba 2, 2021.
Mwenyekiti wa Wakuu wa Vyuo Kanda ya Magharibi, John Nandi ambaye ni Mkuu wa Chuo cha Ualimu Shinyanga, amesema mashindano hayo yatawaongezea wanafunzi wao ujuzi na maarifa katika michezo.
Amesisitiza kuwa dhamira yao ni kuwa na timu bora katika vyuo vyao zitakazokuwa zikifanya vizuri katika tasnia ya michezo kama kauli mbiu ya UMISAVUTA 2021 inavyosema ‘Michezo, Sanaa na Ubunifu kwa Maendeleo ya Uchumi wa Viwanda.
Mkuu wa Chuo cha Ualimu Tabora Balbina Joseph amesema mashindano hayo ni fursa muhimu kwa chuo hicho na vyuo vingine kuzipa uzoefu mkubwa timu zao ili zikafanye vizuri katika mashindano yaliyoko mbele yao.
Jumala vya vyuo vitano vimeshiriki katika mashindano hayo ya Kanda ambavyo ni Kabanga TTC, Kasulu TTC, Tabora TTC, Ndala TTC na Shinyanga (Shycom) TTC.