33.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

WAKURUGENZI HALOTEL, ZANTEL WAENDA JELA

NA Mwandishi wetu


 

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imekuja juu kutetea masafa yake ambayo yalikuwa yakitumiwa isivyo na baadhi ya kampuni za simu zikichomekea kwenye mitandao yao na hivyo kuipa hasara serikali zaidi ya shilingi Bilioni moja kwa matumizi yasiyoruhusiwa.

Zamwizi ni arobaini na waliposhitukiwa viongozi wa kampuni hizo walikiri kufanya makosa hayo ambayo yamesababisha wawili kwenda jela na wengine sita kulipa faini.

Hali hiyo imetokana na TCRA kuweka mitambo mipya ambayo imeweza kutambua udukuzi huo na hivyo kuwakamata wahusika na kuwa peleka mahakamani.

Katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam ikifanya kazi kwa kibali cha Mahakama Kuu imewahukumu watu sita na kampuni mbili, wakiwamo wakurugenzi watendaji wa kampuni za simu za mkononi, Le Van Dai (35) wa Halotel na Sherif El-Barary wa Zantel, kulipa faini ya Sh. milioni 139 au kwenda jela miaka 40 baada ya kukiri tuhuma za uhujumu uchumi.

Katika hali isiyo ya kawaida washtakiwa wote walikiri tuhuma zilizokuwa zinawakabili zikiwamo za kula njama, kuingiza, kufunga mitambo, matumizi ya laini za simu bila usajili wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), na kuisababishia serikali hasara ya Sh. 1,131,936,000.

Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi, Kevin Mhina, baada ya washtakiwa kusomewa mashtaka yao 12 na kukiri makosa aliwahukumu kwa kuwakuta na makosa ya kwenda jela na kufidia hasara iliyotokea kwa Serikali.

Kesi hiyo iliweka historia nchini kwa kutumia muda mchache sana kutokea kusikilizwa kesi hadi hukumu kutolewa kwani Hakimu Mhina aliahirisha kesi hiyo saa 8:05 na kurejea saa 8:30 kuwasomea washtakiwa hukumu na kuwaacha wasikilizaji kesi midomo wazi kwa spidi yake.

Upande wa mashtaka ya Jamhuri uliongozwa na mawakili wa serikali Jacqueline Nyantori na Batilda Mushi ambao waliwataja wahusika  wengine kuwa ni  Lei Cao maarufu kama Peter (28), Huang Yu Meng (27), Msimamizi wa Biashara wa Halotel Zanzibar, Jimmy Mosha (26), Meneja Masoko wa Halotel, Willy Ndoni (29).

Kampuni ya Viettel Tanzania Ltd inafanya biashara kwa jina la Halotel   na Kampuni ya Zanzibar Telecommunication Ltd, maarufu kama Zantel, zote mbili zina makao makuu Wilayani Kinondoni kwenye barabara  ya Ali Hassan Mwinyi  na ile ya Msasani jijini  Dar es Salaam.

Shitaka la kwanza, linadai kati ya Januari Mosi, 2017 na Aprili 30, mwaka huu washitakiwa wa kwanza hadi wa sita, walikula njama ya kutenda kosa la kutumia huduma za mawasiliano kwa njia ya udanganyifu.

Katika shitaka la pili, ilidaiwa kati ya Mei Mosi, 2017 na Aprili 30, mwaka huu, katika jengo la Spring City lililoko Mbezi mshtakiwa wa kwanza hadi wa sita, kwa pamoja walifunga mitambo ya mawasiliano kwa njia ya udanganyifu na kujipatia huduma za mtandao wa Halotel na Zantel bila kibali cha Mamlaka husika ya TCRA .

Shitaka la tatu, nne, tano na sita, linadai kati ya Januari Mosi na Desemba 31, 2017, Aprili 30, mwaka huu jijini Dar es Salaam, mshtakiwa wa tatu na wa nne, waliingiza nchini, waliifunga na kuendesha mitambo ya mawasiliano kwa kuunganisha na kampuni hizo za simu bila kibali cha TCRA.

Shitaka la nane, kati ya Mei Mosi, 2017 na Aprili 30, mwaka huu katika jengo la Spring City, mshtakiwa wa tatu na wa nne, walikutwa wakitumia laini za simu za mkononi zisizosajiliwa na TCRA 281,272 za Halotel na 11,920 za Zantel.

Upande huo wa Jamhuri ulidai katika shitaka la 10 kuwa kati ya Mei, mwaka jana  na Aprili 30, mwaka huu katika matawi ya Zantel ya Dar es Salaam, mshtakiwa wa pili na wa nane walitumia kwa makusudi laini za simu 11,920 zisizokuwa na usajili wa TCRA.

Shitaka la 11 na 12, kati ya Mei Mosi, 2017 na Aprili 30, mwaka huu washtakiwa waliisababishia serikali hasara ya Sh. 1,131,936,400.

Hakimu alisema katika shtaka la kwanza na la pili, washtakiwa wanatakiwa kulipa faini ya Sh. milioni 20 au jela miaka sita na kwa kosa la tatu mpaka la sita, walipe faini ya Sh. milioni 20 au kwenda jela miaka minane.

Kwa kosa la saba mpaka la 10, aliamuru walipe faini ya Sh. milioni 22 au kwenda jela miaka 12 na kwa kosa la 11 na la 12, walipe faini Sh. milioni 20 au kwenda jela miaka 14.

Pia mahakama hiyo ilisema washtakiwa walipe fidia ya zaidi ya Sh. bilioni moja wanayodaiwa kuisababishia serikali hasara na mali zote ikiwamo mitambo na kadi za simu wanazodaiwa kukutwa navyo, washtakiwa viteketezwe.

Pia hakimu aliuamuru upande wa Jamhuri uwarejeshee washtakiwa hati zao za kusafiria, vibali vya kuishi nchini na leseni za biashara.

Vigogo hao walilipa faini kuepuka kifungo, kasoro washtakiwa Lei Cao na Huang Meng ambao walipelekwa gerezani kwa kukosa faini husika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles