24.7 C
Dar es Salaam
Friday, May 17, 2024

Contact us: [email protected]

Viongozi wa Dini wahamasisheni Vijana kufanya kazi kwa weledi-Majaliwa

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ametoa wito kwa viongozi wa dini kuwahimiza vijana kufanya kazi kwa staha, weledi na uadilifu ili kuzitumia rasilimali zilizopo nchini kujiletea maendeleo.

“Nchi yetu imebarikiwa fursa nyingi za kiuchumi, ili jamii ione matunda ya uwepo wa fursa hizo tunategemea sana nguvu kazi ya vijana katika kuzitumia rasilimali zilizopo,” amesema Majaliwa.

Ametoa wito huo leo Jumapili (Oktoba 01, 2023) wakati wa Jubilei ya miaka 125 ya Uinjilishaji katika Jimbo Kuu Katoliki la Songea, kwenye kilima cha Peramiho, Songea mkoani Ruvuma.

Aidha, amezisihi Taasisi za dini kuweka mipango mahsusi na shirikishi ya malezi ya vijana. “Tumieni nafasi zenu kuongeza msukumo wa malezi kwa vijana kwa kuweka mifumo ya kuwafuatilia kwa karibu na kuhimiza ushiriki wao kwenye vyama vya kitume,” amesema Majaliwa.

Kadhalika, Majaliwa amewasihi viongozi wa dini waendelee kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa masuala ya kipaumbele yanayohusu ustawi wa Taifa. 

“Niwasihi sana mtuunge mkono kuhamasisha uhifadhi wa mzingira na matumizi ya nishati safi, kampeni za kupanda miti na usafi wa mazingira, kukemea vikali vitendo vya mmomonyoko wa maadili, matumizi ya madawa ya kulevya na kukemea vitendo vya rushwa”

Katika Hatua nyingine, Waziri Mkuu ameyapongeza madhehebu ya dini kwa kuendelea kutoa huduma mbalimbali za kijamii kwenye sekta za elimu, afya, maji na huduma nyingine za kijamii hasa katika maeneo ya pembezoni.

“Kazi hiyo mnayoifanya ya kutoa huduma kwa jamii ni kuunga mkono dhamira ya Mheshimiwa Dk. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuboresha ustawi wa jamii ya Watanzania kwa kusogeza huduma zote muhimu karibu na wananchi”

Katika Jubilei hiyo, Rais Dkt. Samia ametoa Sh milioni kumi kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 125 ya jubilei ya Uinjilishaji katika jimbo kuu Katoliki la Songea.

Naye, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Songea, Damian Dallu ameishukuru Serikali kwa ushirikiano inaoutoa katika shughuli mbalimbali za huduma za jamii na uinjilishaji zinazofanywa na kanisa katoliki nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles