ABUJA, NIGERIA
CHAMA kikuu cha upinzani nchini Nigeria, Peoples Democratic (PDP) kimesema Rais Muhammadu Buhari hafai kuiongoza nchi hiyo baada ya kusafiri tena kwenda London, Uingereza kwa matibabu.
Buhari (75) alikaa miezi mitano jijini London akitibiwa ugonjwa, ambao haukuwekwa wazi, lakini aliokuwa akiongezewa damu mwilini mara kadhaa.
Aliondoka tena mapema wiki hii, akisema safari hiyo ilitokana na ombi la daktari wake, na kuahidi kurudi Nigeria Jumamosi.
Lakini PDP kimesema katika taarifa yake kuwa ziara hiyo inaonyesha Buhari hayupo sawa kiafya na hivyo hafai kuongoza Taifa.
Kabla ya uchaguzi wa 2015, chama cha PDP, ambacho wakati huo kilikuwa madarakani, kilidai Buhari alikuwa na saratani ya kibofu.
Buhari alikanusha madai hayo akisema ripoti ya matibabu iliyofichuliwa ikionyesha anatibiwa hali hiyo, ilikuwa ya uongo.