27.7 C
Dar es Salaam
Saturday, June 10, 2023

Contact us: [email protected]

MADEREVA HUWA WANAHAMA NA VVU, KUPELEKA KWENYE NDOA

Na LEONARD MANG’OHA


UTAFITI wa kitaifa wa viashiria na matokeo ya Ukimwi nchini wa mwaka 2016/2017 uliolenga kujua hali ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) kitaifa unaonesha kuwa watu 81,000 wenye umri kati ya miaka 15 na 64 hupata maambukizi mapya ya  VVU kwa mwaka. Kwa maana nyingine ni kwamba watu 225 wa umri huo huambukizwa VVU kila siku.

Wanawake ndiyo wanaonekana kuwa waathirika wakuu wa maambukizi hayo, ambapo taarifa zinaonesha kuwa maambukizi mapya kitaifa ni asilimia 0.29, sawa na watu 29 kati ya 10,000.

Wanawake wameambukizwa kwa asilimia 0.40 sawa na wanawake 40 kati ya 10,000 huku wanaume wakiwa ni asilimia 0.17 sawa na 17 kati ya 10,000.

Kiwango cha maambukizi ya VVU kwa ujumla kwa watu wenye umri wa miaka 15 hadi 64 nchini ni asilimia 5.0, wanawake asilimia 6.5 na wanaume asilimia 3.5. Hii ni sawa na kusema kwa wastani watu milioni 1.4 wenye umri wa miaka 15 hadi 64 wanaishi na VVU nchini.

Hali ya maambukizi ya VVU imefikia asilimia 12 kwa wanawake wenye umri wa miaka 45-49 ikilinganishwa na asilimia 8.4 ya wanaume wenye umri kati ya miaka 40-44.

Hali ya maambukizi kwa watu wenye umri wa miaka 15-24 ni asilimia 1.4, lakini kwa wanawake ni asilimia 2.1 na wanaume ni asilimia 0.6.

Hali ya maambukizi ya VVU kati ya wanawake na wanaume ni kubwa zaidi katika kundi la vijana, ambapo maambukizi kwa wanawake wenye umri wa miaka 15-19, 20-24, 25-29, 30-34 na 35-39 ni mara mbili (au zaidi) ikilinganishwa na wanaume wa kundi la umri huo.

KIWANGO CHA MAAMBUKIZI YA VVU KWA UMRI NA JINSI

Kiwango cha maambukizi kwa watu wenye umri wa miaka 15 na zaidi kinatofautiana kati ya mkoa mmoja na mwingine kutoka asilimia 11.4 Mkoa wa Njombe hadi chini ya asilimia moja, mkoani Lindi na Zanzibar.

Kwa mujibu wa taarifa ya Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania Bara (Tacaids), asilimia 52 ya watu wenye umri huo wanaoishi na VVU nchini wamefanikiwa kufubaza virusi hivyo, wanawake wakiwa ni asilimia 57.5 huku wanaume ni asilimia 41.2.

Watu wazima wenye umri kati ya miaka 55 hadi 64 ndiyo wanaotajwa kufubaza zaidi VVU, ambapo wanawake wa umri huo ni asilimia 64 na wanaume ni asilimia 62.

Wanawake wanaonekana kufanya vizuri zaidi katika eneo hili si tu kwa watu wazima bali hata kwa vijana wenye umri kati ya miaka 25-34, ambapo wanawake wamefanikiwa kufubaza VVU kwa asilimia 51 na asilimia 26 tu kwa wanaume.

Mikoa inayofanya vizuri katika eneo hili kwa watu wenye umri wa miaka 15 na zaidi na kiwango cha asilimia kwenye mabano, ni pamoja na Kagera (66), Kilimanjaro (67), Shinyanga (40) na Arusha (29).

 

Lengo la kufikia 90 tatu ifikapo 2020

Lengo la Kitaifa na Kimataifa ni kufikia 90 tatu ifikapo mwaka 2020. Hii inamaanisha kuwa hadi wakati huo asilimia 90 ya watu wanaoishi na VVU wawe wamejua hali yao ya maambukizi.

Asilimia 90 ya waliopimwa na kugundulika kuwa wana maambukizi ya VVU wapatiwe dawa za kufubaza VVU na asilimia 90 ya watu wanaotumia dawa wawe wamefubaza virusi hivyo.

 

Hali ilivyo hadi sasa

Hadi sasa asilimia 52.2 ya watu wanaoishi na VVU wenye umri wa miaka 15-64 wanajua kuwa wameambukizwa, kati yao wanawake ni asilimia 55.9 na wanaume ni asilimia 45.3.

 

Wanaotumia dawa

Miongoni mwa watu hao wanajua hali zao za maambukizi, asilimia 90.9 walithibitisha kuwa wanatumia dawa za kufubaza VVU na kati ya hao wanawake ni asilimia 92.9 na wanaume ni asilimia 86.1.

 

Kufubazwa kwa VVU

Miongoni mwa hao wanaotumia dawa za kufubaza VVU, asilimia 87.7 (zaidi ya watu 87 wamefanikiwa kufubaza virusi hivyo, wanawake wakiwa ni asilimia 89.2 na wanaume asilimia 84.0.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tacaids, Dk. Leonard Maboko, anasema Tanzania imepiga hatua kuelekea kwenye malengo ya 90-90-90 ifikapo 2020, kutokana waliogundulika kuwa na VVU kuanza dawa kwa asilimia 91 ikiwa wamevuka lengo, huku asilimia 88 wakifanikiwa kufubaza VVU.

Anasema kuwa hizo ni dalili njema za kufikia lengo la kufikia sifuri tatu ifikapo 2030. Sifuri hizo zinamaanisha; mosi kutokuwapo kwa maambukizi mapya, pili kusiwe na vifo vitokanavyo na Ukimwi na mwisho ni kuondoa kabisa unyanyapaa na ubaguzi kwa waathirika miongoni mwa jamii.

Hata hivyo, Dk. Maboko anasema pamoja na wanaume kuambikizwa kwa kiasi kidogo ikilinganishwa na wanawake, lakini hawafanyi vizuri katika kutumia dawa za kufubaza VVU. Kwa maneno mengine ni kwamba wanaume ni kama wanakwamisha juhudi za kukabiliana na janga hilo.

 

Juhudi za kufikia malengo haya

Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa tume hiyo, Yassin Abas, anasema ili kufikia malengo hayo, Tacaids inatarajia kuanza kudhibiti maambukizi mapya kwa makundi mbalimbali ikiwamo wavuvi na madereva.

Anasema mpango huo unalenga kukabiliana na maambukizi mapya kutokana na tabia ya maisha ya watu wa maeneo hayo.

Anasema jumla ya Sh milioni 660 zimetengwa kufanikisha mpango huo utakaotekelezwa katika maeneo ya mwambao wa Ziwa Viktoria na visiwa vyake, Ziwa Tanganyika, migodi ya madini iliyopo Simanjiro mkoani Manyara na barabara kuu za kutoka Dar es Salaam kwenda Tunduma, Arusha, Burundi na Rwanda.

“Katika kundi hili la madereva tumewalenga madereva wa masafa marefu kwa sababu ni miongoni mwa makundi hatari kwa kuwa husafiri mara kwa mara na kuwa mbali na familia zao.

“Kwa taarifa yenu, wale madereva wana wapenzi katika kila kituo wanachotembea, kwa hiyo wanahama na Virusi vya Ukimwi na kupeleka katika ndoa zao hivyo, kuziweka katika hatari kubwa ya kuambukizwa,” anasema Abas.

Anasema  hadi sasa tayari wameanzisha vituo vya maarifa vitakavyosaidia kupunguza maambukizi kwa madereva ambapo katika vituo hivyo, watapewa elimu na msaada utakaowakinga na maambukizi ikiwamo kuwapatia kondom na ushauri.

Baadhi ya vituo vilivyojengwa vipo katika maeneo ya Bandari ya Dar es Salaam, Ipogolo mkoani Iringa na stendi ya mabasi ya Tunduma, Manyoni mkoani Singida, Mdaula na Kagongwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,409FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles