Faraja Masinde
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Mkuranga kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi(CCM) Abdallah Ulega, amesema endapo atachaguliwa atahakikisha anaziunganisha Wilaya za Mkuranga na Kibaha kwa barabara yenye hadhi ya mkoa ili kuondoa ulazima wa wananchi wa maeneo hayo kuzungukia jijini Dar es Salaam.
Ulega ameyasema hayo leo Jumatatu Oktoba 12, wakati akizungumza katika muendelezo wa kampeni zake jimboni humo.
Ulega ambaye ni Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi amesema kujengwa kwa barabara hizo kwa kiasi kikubwa kutawezesha kukuza uchumi wa wananchi wa maeneo hayo na Taifa kwa ujumla ambapo amewaomba hao kumpigia kura zote za ndiyo ili akatimize azma yake hiyo.
Amesema barabara hiyo ina umuhimu mkubwa na kwamba endapo itajengwa, kwa asilimia kubwa itawaondolea usumbufu waendaji wa wilaya wakiwemo wasafiri kutoka mikoa ya Morogoro na kwingine ambao kwa sasa huwalazimu kuingia Dar es Salaam kwanza ndipo wafike huko.
“Mtu anayetoka Rufiji, Kibiti au hata mikoa ya kusini na anataka kwenda Kibaha au Morogoro kama hana jambo la kumpeleka Dar es Slaam haitajiki kufika huko, atapita hapa Mkamba, Mzenga, Msanga hadi Mlandizi na kwenda zake Morogoro, kwetu hii itakuwa barabara ya mfano na yenye hadhi,” amesema Ulega.
Amesisitiza kuwa hilo ndiyo lengo lake na Serikali ya CCM ambapo anaamini kwa kukamilika kwake kutawawezesha wananchi wa wilaya hiyo waliopo vijiji vyote vitakavyopitiwa na barabara hiyo kusafirisha mazao yao kwa urahisi na kuwaondolea adha wanayoipata wananchi hao kwa sasa kutokana na kutofunguka kwa barabara hiyo.
Ulega pia amewataka wananchi wa vijiji hivyo kuongeza juhudi ya kilimo kwa kulima mazao mengi ya chakula na biashara ili kujiinua kiuchumi kwa kuwa uhakika wa usafirishaji wa mazao hayo kwenda mikoa mingine utakuwepo kutokana na ujio wa barabara hiyo.