22.4 C
Dar es Salaam
Friday, May 17, 2024

Contact us: [email protected]

TUMUENZI MWALIMU NYERERE KWA VITENDO

TUNAUNGANA na wananchi wote Tanzania kumuenzi na kumkumbuka Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, katika siku ya leo ambayo akifariki dunia kule London, Uingereza.

Hakika alipofariki mnamo Oktoba 14, mwaka 1999, taifa na Watanzania waliachwa katika majozi makubwa, huku wengi wakitafakari jinsi nchi itakavyoendeshwa bila kuwapo kiongozi shupavu na mwadilifu kama alivyokuwa Mwalimu Nyerere.

Hadi kufikia siku ya leo, miaka 18 iliyopita Rais Benjamin Mkapa aliendelea kupokea salamu za rambirambi kutoka kote duniani, ikiwamo Marekani, ambayo ilimtuma Waziri wake wa Mambo ya Nje wakati huo, Madeleine Albright, kuja kushirika katika mazishi ya kitaifa.

Tunapokumbuka siku ya kufa kwake, tunapata pia fursa ya kutafakari maisha yake ya unyoofu, kukumbuka maelekezo na maonyo yake kuhusu mambo mbalimbali, kama vile utawala bora, vita dhidi ya rushwa, maadili ya uongozi na hata mambo ya kimataifa.

Wakati wa ugonjwa wake, kifo na baadaye mazishi ya Mwalimu Nyerere, Watanzania waliungana bila kujali rangi, jinsia, tofauti ya kipato, ukabila na hata dini. Mshikamano waliouonesha Watanzania wakati ule unapaswa kuendelezwa kila inapofika siku hii.

MTANZANIA Jumamosi tunaikumbuka  `Nyerere Day’ huku tukijua kwamba alikufa ‘kifo cha kawaida’, hakuuawa. Si kama Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Mzee Abeid Amani Karume, aliyeuawa kwa kupigwa risasi mnamo Aprili 7, 1972.

Hii inatupa fursa sisi ya kushauri siku hii iadhimishwe katika siku yake ya kuzaliwa, yaani Aprili 13. Hata Mzee Kingunge Ngombale Mwiru aliwahi kupendekeza Nyerere Day ifanyike siku aliyozaliwa Mwalimu. Mashujaa wote duniani hukumbukwa siku waliyokufa ikiwa vifo vyao vilitokana na kuuawa (assassination).

Baadhi ya mashujaa wanaokumbukwa katika siku walizouawa ni pamoja na rais wa 16 wa Marekani, Abraham Lincoln na wa 35, John Kennedy. Wengine ni Mohandas Karamchand Gandhi wa India na Patrice Lumumba wa DRC-Kongo.

Hata Rais mstaafu, Jakaya Kikwete katika hotuba zake alionesha kukubaliana na wazo la kufanya kumbukumbu ya Nyerere siku ya kuzaliwa kwake. Tunasema tumuenzi Nyerere kwa vitendo. Yeye aliishi maisha ya kiasi. Hakujilimbikizia mali.

Tunaambiwa kwamba, Nyerere alishiriki kufyatua matofali wakati wa ujenzi wa Ikulu ndogo ya Chamwino, Dodoma. Tunataka viongozi washiriki kwa vitendo katika kazi wanazozisimamia ili kuongeza ari ya wale wanaowaongoza.

Katika kufanikisha ujenzi wa taifa lenye usawa, Rais huyo wa kwanza wa taifa letu alitaka viongozi na Watanzania wote waitane ‘Ndugu’. Hii ilisaidia kuwafanya wananchi wote wajione sawa na hivyo kuimarisha mshikamano wa kisaikolojia. Mtindo wa viongozi kupenda kuitwa ‘Mheshimiwa’ unatugawa na kutengeneza madaraja kihisia. Kama tunamuenzi Mwalimu, tunashauri basi tuanze sasa kuitana ndugu bila kujali cheo cha mtu.

Katika uongozi wake, Mwalimu Nyerere alisisitiza ujenzi wa maendeleo ya watu, si vitu. Juhudi zinazofanywa na Serikali lazima ziwe ni zile za kumwendeleza binadamu. Haina maana kuwa na maghorofa kama watu wanakosa huduma za afya au pesa mifukoni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles