Na John Walter Babati – Manyara
LICHA ya Serikali kusisitiza wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kupata chakula cha mchana shuleni, baadhi ya shule zimeshindwa kufanya hivyo kwa madai kuwa elimu inatolewa bure.
Shule nyingine hata kwenye vikao vinavyoitishwa kwa ajili ya kuweka utaratibu wa wanafunzi kupata chakula, mwitikio kwa wazazi umekuwa ni mdogo.
Akizungumza na MTANZANIA ofisi kwake hivi majuzi, Mkuu wa Shule ya Sekondari Sigino iliyopo Halmashauri ya Mji wa Babati, mkoani Manyara, Leonardina Binamungu anasema kuwa changamoto kubwa inayokwamisha jitihada za chakula cha mchana shuleni hapo ni ukosefu wa maji.
Kutokana na hali hiyo, huwalazimu kuwaruhusu wanafunzi saa nane mchana hivyo kukosa masomo ya jioni pamoja na michezo, jambo ambalo husababisha ufaulu kuwa mdogo.
''Katika miaka ya nyuma hapa shuleni wanafunzi walikuwa wakipatiwa chakula cha mchana ila tangu serikali iseme hakuna wazazi kuchangishwa, hakuna anayechangia chochote.
"Nadhani kabla ya kutoa agizo hili kwamba wanafunzi wasichangishwe, walipaswa kutembelea na kuangalia mazingira ya shule mbalimbali yalivyo,” alisema Mwalimu Binamungu.
Anasema kuwa ruzuku inayotolewa na Serikali kwa ajili ya kutekeleza sera ya elimu bure katika shule yake imekuwa ni kidogo kutokana na uchache wa wanafunzi.
"Shule hii ni ndogo ina wanafunzi wachache, hii fedha tunayoletewa ya elimu bure ni kubwa kulingana na idadi ya wanafunzi, sasa shule hii ina wanafunzi kidogo na fedha inayoletwa ni kidogo.
“Kifungu cha utawala tunapata Sh 85,000 kati ya hizo 60,000 tunalipa mlinzi, matuimzi ya maji kwa siku katika shule hii ni pipa tatu kwa Sh 15,000,” anafafanua matumizi ya fedha za ruzuku wanazopewa.
Mkuu huyo anaiomba Serikali kutatua changamoto zilizopo hasa shida ya maji waliyonayo ili shule hiyo isonge mbele.
Shule hiyo ina nyumba mbili za walimu huku walimu wakiwa 19 ambapo katia yao wanaoishi kwenye nyumba za walimu ni watano pekee.
"Nafikiri ufumbuzi wa changamoto hizi ni Serikali kuleta maji ya uhakika katika shule hii,"anasema Binamungu.
Katika Halmashauri ya Mji wa Babati, Shule ya Sekondari Sigino pekee ndiyo inayokabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa maji na umeme.
Anaongeza kuwa hadi kufikia Januari 18, mwaka huu, shule ilikuwa na wanafunzi 145; kidato cha kwanza wakiwa 56; wavulana 23 na wasichana 33; kidato cha pili wapo 42 wavulana 19 wasichana 23; kidato cha tatu 24 wavulana tisa, wasichana 18, kidato cha nne 22 wavulana 10, na wasichana 12.
Wakizungumzia adha wanayokumbana nayo kutokana na ukosefu wa huduma ya chakula cha mchana na maji, wanafunzi wa shule hiyo wanasema inawafanya kufanya vibaya katika masomo yao kutokana na kukosa kwa masomo ya jioni kwani inawalazimu kutoka shuleni mapema ili kuwahi majumbani kupata chakula.
Kwa upande wa watoto wa kike wanasema wapo katika hatari ya kupata magonjwa ya kuambukiza kutokana na kukosekana kwa maji vyooni.
"Kuna muda inabidi tuache vipindi tukatafute maji na ni umbali mrefu zaidi ya kilomita tano," anasema mmoja wa wanafunzi wa kidato cha nne ambaye hakupenda jina lake litajwe gazetini.
Anaiomba Serikali itoe msaada katika shule hiyo ili wapate elimu bora na kufanya michezo shuleni.
Akizungumzia suala hilo katika baraza la madiwani katika robo tatu ya mwaka wa fedha 2017\2018 Mkuu wa Wilaya ya Babati, Raymond Mushi anasema wanaendelea kufuatilia shule ambazo hazitoi chakula cha mchana kwa wanafunzi na kuwahamasisha wazazi kuchangia huduma hiyo.
"Chakula kwa wanafunzi ni lazima kitolewe katika kila shule, hii haihusiani na elimu bure hivyo wazazi wanatakiwa wachangie," anasema Mushi.