KAMPALA, Uganda
WAZIRI Mkuu wa Uganda, Ruhakana Rugunda amesema serikali itazisaidia fedha na misaada ya chakula, familia zote zilizopoteza watu na makazi kwenye maporomoko ya ardhi yaliyoikumba nchi hii.
Alitoa ahadi hiyo jana baada ya kuwasili eneo la Naposho katika Wilaya ya Bududa ambalo watu na makazi waliangamia kutokana na maporomoko ya ardhi.
Mpaka sasa Jeshi la Kulinda la Uganda (UPDF), linaendelea kuwatoa watu walionusurika kwenye magofu ya nyumba zilizoporomoka kutokana na mvua kubwa iliyonyesha mwishoni mwa wiki iliyopita katika Wilaya hiyo ya Bududa, Mashariki mwa Uganda.
Inaelezwa kuwa zaidi ya maiti 50 zimekwisha kupatikana.
Habari kutoka katika eneo lililokumbwa na maporomoko hayo zinaeleza mpaka sasa bado mamia ya watu hawajulikani walipo huku maofisa katika wilaya hiyo wakihofia kuwa idadi ya waliofariki dunia huenda ikaongezeka.
Mwandishi wa Shirika la Utanagazaji la Uingereza (BBC), aliyepo eneo alisema wakati wowote Rais Yoweri Museveni alitarajiwa kuwasili mahali hapo kushuhudia maafa yaliyotokea.
Alisema madaraja katika mto Sume na mto Manafwa yamevunjwa na hivyo kulazimu kuwekwa vivuko vya muda hatua ambayo ni hatari .
Serikali imesema vikosi vya uokoaji vimefika katika eneo hilo ingawa miundombinu ya barabara na daraja lililoharibika imesababisha shughuli za uokoaji kuchukua muda mrefu.
Maporomoko mengine ya udongo yalishuhudiwa katika eneo hilo la Bududa mwaka 2010 na yalisababisha vifo vya watu zaidi ya 300.