LONDON,England
UINGEREZA na Marekani zinatafakari kususa mkutano mkubwa wa mataifa unaotarajiwa kufanyika Saudi Arabia.
Ni kutokana na kitendo cha kupotea mwandishi wa habari, Jamal Khashoggi,akiwa katika ubalozi wa nchi hiyo mjini Istanbul, Uturuki.
Khashoggi, ambaye alikuwa mkosoaji mkubwa wa Serikali ya Saudi Arabia, alitoweka tangu Oktoba 2 mwaka huu baada ya kuingia ndani ya ubalozi huo.
Uturuki inaamini kwamba mwandishu huyo aliuawa na makachero wa Saudi Arabia, madai ambayo yanakanushwa na nchi hiyo.
Wakati nchi hizo zikizidi kuvutana, Rais wa Marekani, Donald Trump amekwisha kutangaza kuiadhibu Saudi Arabia endapo ikibainika inahusika.
Pia wafadhili na vyombo vya habari wameshajitoa kuudhamini mkutano huo ambao utafanyika baadaye mwezi huu mjini Riyadh, kwa kile wanachodai ni kuwa na wasiwasi na maisha ya Khashoggi.
Wanadiplomasia walimweleza Mwandishi wa BBC, James Landale kwamba mawaziri wote wawili wa fedha, Steve Mnuchin wa Marekani na Uingereza, Liam Fox huenda wasihudhurie tukio hilo ambalo limeandaliwa na Mwana wa Mfalme, Mohamed bin Salman kuhamasisha ajenda zake mpya.
Msemaji wa Idara ya Biashara ya Uingereza, alisema ratiba ya Dk. Fox bado hajakamilika kwa ajili ya kuhudhuria mkutano huo wa wiki moja.