31.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 11, 2024

Contact us: [email protected]

Safari za ndege Poland hadi Tanzania kuanza

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Rais  Dk. Samia Suluhu Hassan ametoa  maelekezo  ya kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja kutoka Poland  hadi Tanzania.

Akizungumza leo Februari 9,2024 Ikulu, jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari baada mazungumzo na Rais wa Poland, Andrzej Duda, Rais  Samia  amesema  ziara ya rais huyo nchini  ni fursa ya kuimarisha uhusiano zaidi  wa nchi hizo mbili.

Amesema ziara hiyo ni kilelezo kuimarisha uhusiano ulioanza mwaka1962 ikiwa  umetimiza miaka 62.

“Ili kuchochea zaidi utalii na biashara hapa nchini wataalamu wameelekezwa kuchukua hatua zitakazo wezesha  kuanza safari za ndege kutoka Poland hadi Tanzania moja kwa moja, tumeweka ombi letu kwa ukubwa nchini Poland, “amesema Dk. Samia.

Amesema Poland  ni miongoni  mwa nchi 10 ambazo raia wake wengi hutembelea Tanzania  kwa  shughuli za utalii.

Amesema   takwimu zinaonyesha watalii kutoka Poland mwaka 2023 walikuwa 41000 na ndani ya mwezi mmoja mwaka huu wamekuja 6000.

Amesema wamekubaliana na Rais huyo kuimarisha  ushirikiano  uliopo na kuhamasisha uwekezaji zaidi  kwenye sekta za mikakati  kama vile viwanda, madini gesi asilia na uchumi wa buluu.

“Tumeendelea  uhusiano kati ya  Tanzania na Poland katika sekta mbalimbali ikiwemo  kilimo, elimu,  uwekezaji,  utalii, viwanda,  uchumi wa buluu na TEHAMA,”amesema.

Aidha amewakaribisha wawekezaji hususani wa utalii  kuwekeza katika ujenzi  hoteli nchini  kwa kuwa kuna maeneo mazuri  ya uwekezaji  katika uzalishaji.

Naye  Rais wa Poland,  Duda amesema ziara yake nchini imelenga kuibua maeneo mapya ya ushirikiano kati ya nchi hizo mbili na kuleta faida mbeleni.

Amesema  wamekuwa na uhusiano wa miaka 62 na Tanzania na kuimarisha uhusiano wao tangu vita ya pili ya dunia.

“Nitaimarisha uhusiano katika sekta ya utalii na watalii kuendelea kuongezeka kuja kutembelea Tanzania na kushawishi wawekezaji kuja kuwekeza Tanzania kutoka Poland,”amesema Rais Duda.

Amesema kuimarisha sekta ya elimu,  biashara na uchumi  ikiwemo wanafunzi kutoka Tanzania kwenda kusoma Poland katika vyuo  mbalimbali kwa ufadhili  nchi hiyo.

“Vijana watafaidika kusoma katika vyuo hivi watajifunza mambo mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya Tabia Nchi na TEHAMA,  watapata ujuzi wa kutunza vitu hivi,”amesema.

Aidha amemwalika Rais Dk.Samia nchini Poland ikiwa ni fursa ya kuandaa jukwaa  la kuwakutanisha wawekezaji nchini humo kujadili fursa za uwekezaji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles