TIMOTHY ITEMBE
MKUU wa Mkoa Mara, Adam Malima ametaja sababu za kuongezeka matukio ya ubakaji kwa kipindi cha Januari hadi Mei mwaka huu.
Amesema hiyo inatokana na baadhi ya walimu wasiokuwa na maadili kuwafanyia wanafunzi wao vitendo hivyo pamoja na waendesha pikipiki maarufu (bodaboda).
Malima alisema kipindi cha Januari hadio Mei mwaka huu kuna matukio ya vitendo vya ubakaji zaidi ya 12 vimeripotiwa ofisini kwake ili kuvishugulikia na kupatiwa ufumbuzi.
Alisema waathirika katika vitendo hivyo ni wanafunzi wa shule za misngi na sekondari.
RC alitaja ongezeko la vitendo hivyo kuwa vinachangiwa na baadhi ya walimu wa shule za msingi na sekondari na waendesha pikipiki.
Matukio ya ukatili na ubakaji yakiwamo ya ulawiti ni miongoni mwa ukiukwaji wa sheria na haki za binadamu na utawala bora nchini.
Alisema kuenea kwa vitendo hivyo kunasababisha uzorotaji maendeleo kwa taifa.
“Ofisini kwangu kumeripotiwa kesi za ubakaji zaidi ya 12 baadhi zikiwa zinahusisha walimu wa shule za misngi na sekondari.
“Niwaombe ndugu zangu haki ya kufanya kazi bila kubugudhiwa ni ya msingi lakini niwatake kuacha vitendo vya rushwa ya ngono kazini pamoja na vitendo vya ubakaji watoto wa shule,” alisema Malima.
RC alitaja vipaumbele katika mkoa kuwa ni elimu, afya, miundombinu ya barabara na maji.
Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Tanzania Mkoa Mara, Livingstone Gamba aliwataka walimu na wafanyakazi kwa ujumla kuchukua wajibu wa kufanyakazi kama sheria inavyowataka.