26.2 C
Dar es Salaam
Saturday, May 18, 2024

Contact us: [email protected]

Rais Samia: Wanasiasa msiingilie mashirika ya umma

*Atoa onyo kwa MA-CEO watakaoua mashirika

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, amewataka wadau na wanasiasa kuacha tabia ya kuingilia uendeshaji wa mashirika ya umma nchini ili yajiendeshe kwa mafanikio.

Rais Dk. Samia ameyasema hayo leo Jumamosi Agosti 19, 2023 jijini Arusha alipokuwa akifungua Kikao Kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma kinachofanyika leo katika Ukumbi wa AICC – Arusha.

“Naomba hii tabia ya kuingiza siasa kwenye uendeshaji wa mashirika ya umma kwa sababu hatua hii si afya kwa mashirika haya na kufanya yajiendeshe kwa kusua sua na kuleta hasara kubwa,” amesema Rais Dk. Samia kweye ufunguzi wa kikao kazi cha wenyeviti wa bodi na watendaji wakuu wa taasisi za Umma kinachofanyika jijini Arusha kutafuta njia za kuboresha uendeshaji wa mashirika ya umma nchini Tanzania.

MASHIRIKA YA UMMA YAUZE HISA KWA WANANCHI

Aidha, Rais Dk. Samia ameyataka mashirika ya umma kurejea utaratibu wa kuuza hisa kwa wananchi ili kuwapa umuliki.

“Nataka niseme kidogo kuhusu azma ya kuanzisha mashirika haya ya umma. Wakati wa Mwalimu Nyerere alivyoanzisha Mashirika haya ya umma, alitaka yamilikiwe na wananchi wenyewe kupitia hisa kama Public Enterprises na siyo Government Enterprises. Tunajiita Mashirika ya Umma lakini dhana ya Mashirika ya Umma, ni mashirika ambayo umma Watanzania wana hisa katika mashirika yale.

“Mashirika yakajitafakari na yale ambayo yanaweza kurudi sokoni kwa wananchi na kuuza hisa zake ziuze ili wananchi wawe na umiliki. Nataka Watanzania warejee kwenye utaratibu wa kununua hisa za mashirika yetu ya umma kama ilivyokuwa zamani. Kuna mashirika ambayo yangeweza kuuza hisa zake. Kwa sasa wapo wananchi wenye uwezo wa kununua hisa hata kama ni kidogo kidogo,” amesema Rais Dk. Samia.

KUANZISHA MFUKO WA UWEKEZAJI WA UMMA

Sambamba na hayo Rais Dk. Samia amesema Serikali yake inaanzisha mfuko wa uwekezaji wa umma kupunguza utegemezi wa mashirika ya umma kwa serikali.

“Serikali imepanga kuanzisha mfuko wa uwekezaji wa umma kama njia ya kupunguza utegemezi (wa mashirika ya umma kwa Serikali) tukiamini mpango huu utakuwa na faida kubwa kwa nchi yetu,” amesema Dk. Samia.

ONYO KWA WAKURUGENZI

Dk. Samia pia amewataka Wakurugenzi wa Mashirika ya umma kujiandaa kisaikolojia, akisema kuwa shirika lolote litakalo kufa, litaondoka na nafasi ya Mkurugenzi wake.

“Ujumbe kwa M-CEO wa Mashirika ya Umma, shirika likifa, nawe utalazimika kupoteza nafasi yako kwa sababu mkakati tuliokuwa nao kama Taifa ni kufanikisha dira na maendeleo kwa kupitia nyanja mbalimbali yakiwemo mashirika ya umma ambayo leo tumekuja hapa kujadili ufanisi wake. Shirika likifa kufa nalo,” amesema Dk. Samia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles