24.1 C
Dar es Salaam
Sunday, September 8, 2024

Contact us: [email protected]

“Mradi wa vipepeo ndio tunataka kusikia”-Wananchi Muheza

Na Faraja Masinde, Mtanzania Digital

Wananchi wilayani Muheza mkoani Tanga wameiomba Serikali kuangalia namna ya kuondoa zuio la kusafirisha vipepeo nje ya nchi kwani mradi huo ulikuwa ukiwasaidia kujikwamua kiuchumi.

Aloyce Elia Mwenyekiti wa Kijiji cha Msasa IBC akizungumza na Waandishi wa Habari(hawapo pichani)

Wananchi hao wametoa ombi hilo hivi karibuni baada ya timu ya Waandishi wa Habari ambao ni Wanachama wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) kutembelea milima ya asili ya Amani iliyoko wilayani Muheza mkoani Tanga na kusikiliza kilio cha wananchi ambao walikuwa wananufaika na mradi huo kabla ya kustishwa Machi 17, 2016.

Aloyce Elia ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Msasa IBC, wilayani Muheza ambapo amesema kuwa wanaiomba Serikali kuangalia tena zuio hilo kwani ulikuwa ukiongeza pato la mwananchi mmoja mmoja hivyo kusaidia kuendesha maisha yao ikiwemo kusomesha watoto.

“Mradi wa vipepeo ulikuwa unasaidia sana katika jamii za vijiji karibu saba vinavyozunguka ushoroba wa Derema ambapo kipato cha mtu mmoja mmoja kilikuwa kikiongezeka.

“Ukiangalia upande wa jamii, kuna fedha ambazo zilikuwa zinapatikana kutoka kwenye pato la mradi wenyewe (7%) mfano sisi katika kijiji chetu tuliweza kujenga ofisi ya kijiji pamoja na choo.

“Pia, katika kijiji cha Antakae waliweza kutumia fedha za mradi huo kununua shamba ambalo kwasasa wamejenga shule, ukija kijiji cha Kisiwani wamepata maji safi, Kwazitu wamepata chumba cha darasa na vyoo vya shule.

“Kwa hiyo huu ni mradi ambao umesaidia sana jamii yetu, waliokuwa hawana nyumba nzuri wamejenga, waliokuwa hawana usafiri wamenunua pikipiki.

“Hivyo, kitendo cha kufikia kwamba mradi huu umestishwa na Serikali ilileta simanzi kubwa sana kwa wananchi lakini pia kipato chao kilipungua sana,” amesema.

Ameongeza kuwa iwapo mradi huo ukirudi hata leo wapo tayari kuupokea kwa asilimia 100 kwani ni mkombozi wa maisha yao.

“Mradi huu ukirudi tuko tayari kuupokea kwa asilimia 100 na siyo mimi tu ni wote tuko tayari kwani kila mtu utakaye mwambia anasema huu ndiyo mradi tunaotaka kusikia,” amesema.

Upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Magoda kilichopo kata ya Kisiwani Tarafa ya Amani, amesema wao kama walinzi wa shoroba wanaomba kurudishiwa mradi huo wa vipepeo kwani utawapunguzia machungu na makali ya maisha.

“Tunamuomba Waziri wa Maliasili na Utalii kwa nia njema kabisa kwamba aturudishie mradi wa vipepeo kwani wananchi wa tumekuwa wahanaga katika kuulinda msitu huu wa Amani.

“Wananchi tulikuwa tayari tumeshajipangia maeneo yetu kwa ajili ya kupata mbegu na tulishapata utaalamu wa namna ya kutenga mayai na kila kitu, hivyo mradi ule hata mtu wa miaka 80 alikuwa anaweza kufanya bila shida ndiyo sababu baada ya kustishwa tuliathirika sana,” amesema.

Naye, Mtendaji wa Kijiji cha Magoda, Betty Simuhappy amesema wananchi wake walikuwa wakinufaika kwa kipindi kirefu kabla ya kustishwa kwa mradi huo.

“Mradi huu ulikuwa na msaada sana kwetu lakini baada ya kustishwa imekuwa changamoto na imefikia hatua wananchi wanaingia ndani ya hifadhi na kuiba, hivyo Serikali iangalie namna ya kuurejesha ili kusaidia wananchi,” amesema Betty.

Hata hivyo, wakati wananchi hao wakiwa bado katika mtanziko huo juu ya lini biashara hiyo ya uuzaji wa Pupa itaendelea, Serikali imebainisha kuwa wanapaswa kuendelea kuwa wavumilivu.

Mapema Jumatatu, Mkurugenzi wa Wanyamapori wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Fortunat Msofe amenukuliwa na Gazeti la Serikali la Daily News akisema kuwa wanaendelea na jitihada za kutatua suala hilo huku akiwaomba wakulima hao kuwa na subira.

Aidha, imesisitiza kuwa inapitia faida na hasara iliyopatikana kutokana na mauzo ya wanyamapori hai kabla ya kufanya uamuzi wa mwisho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles