Na FATUMA SAID
RAIA 19 wa Ethiopia wamekamatwa polisi mkoani Mwanza kwa kuingia nchini kinyume cha sheria .
Kamanda wa Polisi Mkoa Mwanza, Jumanne Muliro alisema juzi kuwa raia hao walikamatwa Machi 19, mwaka huu katika mtaa wa Amani Kata ya Butimba Wilaya ya Nyamagana.
Alisema walikamatwa nyumbani kwa Benedictor Gervas (57) mkazi wa mtaa huo kwenye chumba alichokuwa amepanga mtuhumiwa Manka Kagulu (21).
Kamanda aliwataja raia hao kues ni Alemu Ayule, Degefa Tesfaye, Tsededke Tumisdo, Miratu Labebeu, Sirgage Kemela,Temesgen Dekeyo, Zeleke Dascelegn,Tasela Feyis,Takape Ayeke,
Wengine ni Zamachu Mathewos, Eshatu Mangasha, Salamu Barekato, Makome Abeba, Amaneui Abana,Gaytso Arflca,Kebamo Gathey, Wondemu Xadesu, Nageshe Ayeye na Degefe Abebe.
“Jeshi la polisi linafanya utaratibu wa kumpata mkalimani kuweza kubaini sehemu wanayotoka na wanapokwenda.
“Hivyo watuhumiwa hao wanafanyiwa taratibu za kufikishwa idara ya uhamiaji hatua nyingine za sheria ziweze kuchukuliwa,”alisema Muliro.
Kamanda Muliro alisema pia kuwa polisi wanawashikilia waganga 16 wa kienyeji wanaopiga ramli chonganishi katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mwanza.
Alisema miongoni mwao, sita ni wanaume na wanawake ni 10 (majina yanahifadhiwa kwa upelelezi) .
Vilevile, alisema polisi wamewakamata watuhumiwa sugu nane wanaojihusisha na matukio makubwa ya uhalifu wakiwa katika hatua za awali kwa kupanga njama ya kutenda vitendo vya uhalifu.
Alisema maji ya watu hao yameifadhiwa kwa uchunguzi zaidi na watafikishwa mahakamani pale taratibu za sheria zitakapokamilika.
Kamanda Muliro ametoa wito kwa wanachi kutoa taarifa mapema wanapoona vitendo viovu vinafanyika maeneo yao polisi waweze kufika mapema na kuzuia uhalifu kutendeka.