NORA DAMIAN na LEONARD MANG’OHA, DAR ES SALAAM
SIKU moja baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, kutaka Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT – Wazalendo), ajisalimishe polisi ndani ya siku mbili, Jeshi la Polisi limesema limeanza kumchunguza mwanasiasa huyo.
Juzi Waziri Lugola alimtaka mbunge huyo kujisalimisha kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, vinginevyo atamwagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro amkamate.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Msemaji wa Jeshi la Polisi, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Barnabas Mwakalukwa, alisema tayari wamefungua jalada la uchunguzi dhidi ya mbunge huyo.
“Tutafanya uchunguzi kuhusu tuhuma zinazomkabili Zitto kwa kuzingatia utawala wa sheria.
“Kama tutapata ushahidi wa kutosheleza tutakapomuhitaji kwa hatua za upelelezi tutamwita na atakwenda kuripoti Lindi,” alisema Mwakalukwa.
Kwa mujibu wa Lugola, mbunge huyo alitumia lugha ya matusi dhidi ya viongozi na amekiuka agizo la Rais la kutaka wanasiasa kutofanya mikutano nje ya maeneo yao.
Julai 29 Zitto alifika kwenye mkutano ulioandaliwa na Mbunge wa Kilwa Kusini, Selemani Bungara maarufu Bwege (CUF) na kuhutubia.
Hata hivyo Zitto juzi aliandika katika ukurasa wake wa Twitter akisema kwamba waziri hana mamlaka ya kumtaka ajisalimishe polisi na kama polisi wanamtaka watoe wito wa kisheria atakwenda.
HAKUNA MBWA ALIYEPOTEA
Jeshi hilo limesema hakuna mbwa aliyepotea bali kulikuwa na mkanganyiko na mbwa anayedaiwa kutoweka alikuwa kwenye mafunzo katika Bwalo la Maofisa wa Polisi Oysterbay.
Mwakalukwa alisema mbwa Hobi aliyetajwa awali alikuwepo makao makuu ya kikosi hicho na ambaye hakuwepo ni Gilo aliyekuwa akiendelea na mafunzo Oysterbay.
Katika mkutano huo jeshi hilo liliwaonyesha waandishi wa habari mbwa hao na kuutaka umma uendelee kuwaamini kwani mbwa wote wako salama na wanaendelea na kazi zao za kila siku.
“Movement za mbwa wa polisi hazipaswi kuelezwa kwenye vyombo vya habari kwa sababu hii ni mikakati yetu, lakini kwa sababu ya mkanganyiko ndio maana tunawaambia.
“Hata ‘movement’ za mbwa si lazima kila askari ajue, inawezekana mheshimiwa (Waziri Lugola) alimuuliza askari ambaye hajui,” alisema Mwakalukwa.
Naye Kamanda wa Kikosi cha Mbwa na Farasi, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Egyne Emmanuel, alisema bandarini kuna mbwa sita wakiwamo Hobi, Gilo na Baxe.
“Wakati Waziri alipokwenda bandarini Hobi na Baxe walikuwa hapa (makao makuu ya kikosi hicho), kwa sababu kule bandarini kuna ujenzi unaendelea na vyumba vilikuwa havitoshi hivyo walikuwa wanang’atana,” alisema Kamanda Emmanuel.
Katika hatua nyingine Chama cha ACT-Wazalendo, kimemshauri Waziri Lugola, kuchunga kinywa chake kwa sababu baadhi ya kauli zake zinaleta ukakasi na hazikubaliki kwenye utawala wa haki.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Katibu wa Itikadi, Mawasiliano na Uenezi wa chama hicho, Ado Shaibu, wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Alisema nchi haiendeshwi kwa matamko hivyo Waziri Lugola ni muhimu ajiridhishe kuhusu mipaka ya madaraka yake na matakwa ya kisheria juu ya masuala mbalimbali kabla ya kuyatolea matamko.
Shaibu alisema kutokana na unyeti wa wizara anayoiongoza inayogusa haki na utu wa watu anapaswa kupunguza papara katika kuitumikia.
“Tunayasema haya kwa kurejea matamshi yake mbalimbali ya hivi karibuni mfano kudharau kwake kupotea kwa mwandishi wa habari Azory Gwanda na kitisho chake kwamba wanasiasa wataokiuka maelekezo yake atawapasua matumbo.
“Ni muhimu achunge kinywa chake kwa sababu baadhi ya kauli zake zinaleta ukakasi na hazikubaliki kwenye utawala wa haki” alisema Shaibu.
Alisema chama chake kimemtaka Zitto kuendelea na majukumu yake na kulipuuza agizo la Lugola la kumtaka aripoti polisi ndani ya siku mbili kwa sababu limetolewa kisiasa kwani hana mamlaka ya kufanya hivyo.
Shaibu alisema wito wa kuitwa polisi ni wa kisheria na unapaswa kutolewa na Jeshi la Polisi na si vinginevyo.
“Chama chetu kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii kimepata taarifa juu ya agizo la Waziri Lugola akimtaka kiongozi wa chama chetu Zitto Kabwe, kuripoti polisi mkoani Lindi baada ya Zitto kuwa amealikwa na Mbunge wa Kilwa Kusini, Suleiman Bungara (CUF), kuhutubia wananchi wa Kilwa Masoko Julai 29 mwaka huu.
“Baada ya wanasheria wa chama kuyapitia matamshi ya Waziri Lugola na kujiridhisha kwamba hayana msingi wa kisheria, chama kilimwelekeza Kiongozi wa Chama kuendelea na majukumu yake hadi hapo utakapotolewa wito halali wa Jeshi la Polisi” alisema Shaibu.
Aliongeza kuwa Kiongozi wao hawezi kuwajibika kwa wito wa kisiasa kwa sabau hakuna sheria inayomzuia mbunge wa jimbo moja kumwalika mbunge wa jimbo jingine kuhutubia katika mkutano wake ilimradi mkutano husika umefuata taratibu za kisheria katika kuitishwa kwake.