30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Polepole awaonya wakuu wa mikoa wasaka ubunge

NA MWANDISHI WETU -DAR ES SALAAM

KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole ameonya baadhi ya wakuu wa mikoa kutaka kugombea ubunge hali ya kuwa kazi waliyopewa hawajamaliza.

Polepole alisema hatua ya viongozi hao kuwa na mpango wa kugombea ubunge ni kwenda kunyume na agizo la Mwenyekiti wa CCM, Rais Dk. John Magufuli.

Hadi sasa majina ya wakuu ya mikoa ambayo yamekuwa yakitajwa kwenye mbio za ubunge ni Paul Makonda anayedaiwa kutaka kugombea Jimbo la Kigamboni, Ally Happy (Kondoa Mjini) na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo ambaye naye anatajwa kulitaka Jimbo la Arusha Mjini.

Juni 13 mwaka huu, CCM kupitia katibu huyo wa Itikadi na Uenezi wakati akitangaza ratiba ya mchakato wa uchaguzi, alisema wanaowania ubunge, uwakilishi na udiwani wanapaswa kuzingatia katiba, sheria za uchaguzi na miongozo ya chama hicho.

Pia alisema mchakato wa uteuzi wao wa wagombea utatangazwa Julai 11 na kwamba wavurugaji watakaojipeleka mbele kutafuta uongozi, watawasaidia kwa kuwakata mapema kwa kuwa CCM ya sasa sio ya mchezo na haina mzaha.

Hivi karibuni akizungumza na wanachama wa CCM Wilaya ya Kigamboni, Polepole aliwataka kupeleka salamu kwa mkuu wa mkoa ambaye alidai anao madalali wanampigia kampeni ili aweze kupigiwa kura.

Alisema tayari amesikia kuna wakuu wa mikoa wameweka madalali kwa jimbo hilo na kwamba wanajipitishapitisha hivyo wawafikishie salamu kwa sababu watawakata.

“Sasa madalali naomba mnifikishie salamu, sio uongo kwa sababu kwenye kukata na mimi pale nipo, na tunapokuwa tunakata ni hoja na mimi nitasema huyu namjua na dalali wake namjua na nilijulisha kwenye sekretarieti huyu ni mvurugaji, nasema huyu akatwe halafu mjadala.

“Na mwisho mimi nitatumia turufu na turufu ni kusema mkimuweka huyu nitakwenda kuibua kwenye Kamati Kuu kwa sababu kwenye sekretarieti sisi ndio tunatengeneza ajenda za Kamati Kuu.

“Kamati Kuu anaongea katibu mkuu kama sisi ni ufafafuzi, akipita mtu wa ovyo namjua na wengine hawamjui tunakaa naye kwenye Kamati Kuu na kwenye Kamati Kuu Rais Magufuli hakosei, yuko amenyooka,” alisema Polepole.

Aliwataka wanachama hao kuwaogopa kama ukoma wanaojipeleka mbele kuutafuta uongozi.

“Anayejipeleka mbele kuutafuta uongozi mwogopeni kama ukoma, uongozi mtu hupewa na tunapompatia lazima uwe mnyenyekevu kwa sababu tumekupa na hukustahili.

“Mtu anayejipeka mbele hatuheshimu sisi na chama chetu kwa sababu uongozi anautaka yeye, kiongozi ni mtumishi, ni lazima uwe mnyenyekevu kwa sababu kazi hiyo tumekupa kwa muda na ukikosea tunachukua tena, ndiyo maana inaitwa dhamana.

“Sasa nimesikia hapa Kigomboni mambo ya kihuni kwamba mnawatafutia watu ubunge wakuu wa mikoa, nasikia hilo liko hapa, eti kuna wakuu wa mikoa wanataka ubunge hapa.

“Basi nipelekeeni salamu wasithubutu, wasijaribu kwa sababu mambo mawili tutafanya na haya maneno sio yangu, ni mwenyekiti wa chama na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ndiye msemaji wa chama, mimi nafanya tu kwa niaba yake, ukipewa ukuu wa mkoa uwe na nidhamu na adabu na heshima.

“Tumekuona utusaidie hapo, kazi huchagui ukipewa kaa nayo, ishi nayo kufa nayo, ukianza kuwa na tamaa… tamaa ya kwenda ambako hukutumwa wewe ni mlafi, kwenye kanuni ya maadili kiongozi lazima awe mtu anayetosheka, usiwe mtu mwenye tamaa kila kinachopita unakitaka wewe, utaharibikiwa siku moja.

“Kama ukipewa ukuu wa mkoa ridhika, sijasikia mkuu wa wilaya, sijasikia mama, endelea kuchapa kazi, sijasikia habari zako ila nimesikia kuna wakuu wa mikoa wanataka jimbo hapa kana kwamba ni lao wanakuja kuchukua hapa, tosheka umepewa kazi ya ukuu wa mkoa, umemaliza na kutatua kero?

“Sasa mara chache huwa napenda kutumia neno hili, koma kama ulivyokoma kunyonya ziwa la mama yako,” alionya Polepole.

Aliwaeleza wanachama hao kwamba wakiruhusu watu wenye tamaa ya kutaka kila wanachokitaka chama kitakuwa holela.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles