Na Brighiter Masaki, Mtanzania Digital
WASANII wanaotamba katika Bongo Fleva nchini, Faustina Charles ‘Nandy’ na Zuhura Othuman ‘Zuchu’, wameingia kwenye mchuano wa kuwania tuzo za AFRIMMA kipengele cha msanii bora wa kike Afrika Mashariki .
Kutokana na mchuano huo, wasanii hao wameanza kuwagawa mashabiki katika mitandao ya kijamii kila mmoja akiwa na timu yake inayohamasisha kumpigia kura.
Hali hiyo inatokana na wanadada hao kuachia nyimbo kali hivi karibuni, zinazoonekana kupendwa na kuwa na mashabiki wengi.
Nandy anatamba na kibao chake cha ‘Acha Lizame’ alichomshirikisha Harmonize, wakati Zuchu akitamba na wimbo wa Nisamehe.
Tofauti na Zunchu na Nandy, katika kipengele hicho pia wapo wasanii wengine wa Afrika Mashariki kama vile Nadia Mukami (Kenya), Tanasha Donna (Kenya), Maua Sama (Tanzania), Rosa Ree (Tanzania), Vimka (Uganda) na wengine wengi.
Tuzo hizo zilizokuwa na vipengele mbalimbali, zinatarajiwa kutolewa Novemba 15, mwaka huu nchini Marekani.