MOROGOROÂ NA LILIAN JUSTICE
WATU watatu wamefariki dunia mkoani Morogoro katika maeneo tofauti ikiwamo mwanaume kumuua mkewe kwa kutumia kitu chenye ncha kali kichwani kabla ya kujinyonga na mwingine  kuuawa kwa kupigwa kichwani  na usoni na kitu butu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mtafungwa alisema   tukio la kwanza lilitokea  Julai 28 mwaka huu  asubuhi  katika eneo la Njage Tarafa ya Mngeta wilayani Kilombero.
Alisema  Rose Mngwe (43) mkazi wa Njage aliuawa na mumewe, Jacob Kambo kwa kukatwa na shoka  kichwani  kabla ya mumewe huyo kujinyonga kwenye mti kwa kutumia kamba .
Ilielezwa  chanzo cha mauaji hayo ni mgogoro wa  familia na tayari miili ya wanandoa hao imekwisha kufanyiwa uchunguzi kwa ajili ya kufanya utaratibu wa mazishi.
Tukio la pili lilitokea  ulai 30 mwaka huu   alfajiri maeneo ya Kitongoji cha Igagafu Kijiji cha Msowero wilayani Kilosa ambako  mzee Leo Charles ( 61) mkazi wa Igagafu aliuawa kwa kupigwa na kitu butu  kichwani na usoni na mwanae,   Emanuel Charles.
Kamanda Mtafungwa alisema  mtuhumiwa alikamatwa  na atafikishwa mahakamani  uchunguzi utakapokamilika.
Alitoa wito kwa wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi na   kuepuka msongo wa mawazo unaosababisha kujidhuru.