23.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

VIJANA WAJASIRIAMALI WAPEWA MAFUNZO

 

Na JANETH MUSHI, ARUSHA


VIJANA wajasiriamali kutoka Kata tatu zilizopo Halmashauri ya Jiji la Arusha wamepatiwa mafunzo ya ujasiriamali na utambuzi wa fursa zilizopo katika maeneo yao.

Wajasiriamali hao kutoka Kata za Sokoni One, Lemara na Unga Ltd, wametakiwa kutumia vema fursa za mafunzo hayo ya ujasiriamali katika kujiongezea kipato, ikiwa ni pamoja na kushiriki katika utungaji na utekelezaji wa sera za vijana katika maeneo yao.

Hayo yalisemwa jana jijini hapa na Mratibu wa mradi wa vijana unaotekelezwa na Taasisi ya  Arusha Municipal Foundation, Stanley Humbo, mradi unaofadhiliwa na Foundation For Civil Society, wakati akizungumza katika mafunzo ya siku mbili kwa vijana hao.

Alisema katika mafunzo hayo ya siku mbili wameweza kuwafundisha vijana hao masuala mbalimbali ya ujasiriamali, kuwawezesha kiuchumi na kujadili changamoto zinazowakabili na njia mbadala ya kuzitatua.

Alisema lengo la mradi huo ni kuwasaidia vijana na kuwawezesha katika masuala yanayogusa changamoto zao, kuwawezesha kuzifuatilia na kutambua fursa mbalimbali zinazowazunguka katika maeneo yao kuanzia ngazi za chini.

Alitaja malengo mengine ya mradi huo kuwa ni kuwasaidia vijana kushiriki katika masuala ya maamuzi kuanzia ngazi za chini hadi Taifa.

“Tunajaribu kuwaunganisha vijana na taarifa muhimu ambazo zinagusa maslahi yao na kuwaunganisha na taasisi mbalimbali, ikiwamo Serikali na sekta binafsi kama SIDO, TCCIA na Halmashauri ya Jiji, hivyo tunawaomba kupitia mafunzo haya mtumie fursa mnazopata kuanzisha shughuli za kujiongezea kipato,” alisema.

Alisema mradi huo unaotekelezwa katika kata tatu zilizopo jijini hapa, unatekelezwa kwa kutumia mfumo wa mabaraza ya vijana katika kila kata, lengo likiwa ni kuwarahisishia vijana kupata fursa mbalimbali za kiuchumi.

Mmoja wa washiriki hao, Julius Meyasi, kutoka Kata ya Sokoni One, alisema hiyo ni mara yake ya 11 kushiriki mafunzo ya aina hiyo na kwamba awali hakuweza kujua masuala ya sera, mikopo kwa vijana na ujasiriamali kwa ujumla, lakini baada ya kushiriki aliweza kuanzisha biashara ya fedha.

“Kwa sasa ninajihusisha na biashara za kifedha, yaani m’pesa na tigopesa pamoja na ufugaji kuku ambao awali niliujaribu ila nilishindwa na kuku wote wakafa, kwa sababu sikuwa na elimu yoyote, ila sasa hivi nimeweza kuwafuga kutokana na elimu niliyopata,” alisema.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles