HOSPITALI ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kupitia Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, imefanikiwa kufanya upasuaji mkubwa wa moyo kwa mara ya kwanza tangu ianzishwe.
Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi jana kwa njia ya simu Kaimu Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Profesa Mohamed Janabi, alisema upasuaji huo ulifanyika kwa saa nne hadi tano hadi kuamka.
“Ni operation (upasuaji) mkubwa sana kufanywa hapa kwetu, awali tulimpokea mgonjwa na kumfanyia vipimo ambapo tuligundua mishipa yake mitatu ime-‘block’(imeziba) kwenye moyo,” alisema Profesa Janabi.
Profesa Janabi alisema kutokana na ugunduzi huo iliwalazimu timu ya madaktari na manesi kutoka nchini pamoja na wenzao kutoka Saudi Arabia kushirikiana kupandikiza mishipa na kufanya upasuaji.
“Ilibidi kutoa mshipa mmoja mguuni na kuupandikiza kifuani hadi kwenye moyo, tulikuwa na timu kubwa kama ya watu 10 na tunategemea kuendelea zaidi,” alisema Profesa Janabi.