33.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

MRADI WA EP4R ULIVYOPUNGUZA MIMBA, UTORO SHULENI

Na ASHA BANI – aliyekuwa Lindi


MRADI wa Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R) unaolenga kuboresha hali ya elimu nchini umezaa matunda katika mikoa ya kusini.

Mradi huo unaoratibiwa na kusimamiwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, umesaidia kupunguza utoro shuleni, idadi ya wanaopata mimba kwa watoto wa kike na hata mazingira bora ya kufundisha na kujifunzia kwa wanafunzi na walimu.

Mradi huo uliofanikiwa katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, sasa umegeukia mikoa ya Kusini lengo likiwa ni kuhakikisha shule zinakuwa na mazingira bora yatakayohamasisha wanafunzi kupenda kuhudhuria masomo.

Mkoani Lindi,  zimetengwa Sh bilioni 2.8 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa shule mbalimbali yakiwamo mabweni, nyumba za walimu, matundu ya vyoo na madarasa. Katika baadhi ya shule kumeongezwa madarasa kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha tano na sita.

Akitoa mchanganuo wa matumizi ya fedha hizo, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi, anasema tayari shule 12 za msingi zimekarabatiwa.

Anazitaja shule hizo kuwa ni Nangumbu, Nachiungo, Mnamba, Masoko, Rushungi, Kikanda, Singino, Kitomanga na Dimba.

Nyingine ni Kilimahewa, Ngwenya na Mkwajuni.

Anasema fedha hizo pia zimekarabati shule saba za sekondari ambazo ni Narungombe, Ruangwa, Nkowe, Kilwa, Ilulu, Kitomanga na Nachingwea Day, zilizopo Halmashauri ya Ruangwa.

Zambi anasema jumla ya madarasa 30 yamekarabatiwa na 32 kati ya 47 yameshakamilika. Anasema kwa upande wa matundu ya vyoo; 84 kati ya 114 yameshakamilika, huku vyumba vya madarasa 15 na matundu ya vyoo 30 vikiendelea kujengwa.

Akizungumzia shule za sekondari, anasema jumla ya madarasa matano yamekarabatiwa na 22 yamejengwa, maabara sita, wakati matundu ya vyoo 52 kati ya 62 yameshakamilika.

Anasema madarasa sita, matundu vyoo 10 na mabweni nane yanaendelea kujengwa.

“Ukarabati huu umesaidia kupunguza utoro, kuongeza ufaulu, hata wale wanafunzi wa kike waliokuwa hawafiki shuleni pindi wanapokuwa hedhi kutokana na uhaba wa matundu ya vyoo sasa wanakuja na wanafaulu vizuri,” anasema Zambi.

Anasema ukarabati wa maabara kwa mkoa huo umewasaidia wanafunzi wanaosoma masomo ya sayansi, sasa hivi wanasoma kwa vitendo na hivyo kuwafanya waelewe kwa urahisi.

Anasema bado mwitikio wa elimu  katika mkoa huo uko chini kutokana na wazazi/walezi kutowahimiza watoto wao kupenda shule badala yake wanaendekeza mila na desturi kama unyago na jando ambazo hazina manufaa kwao.

Mwalimu Mkuu msaidizi wa Shule ya Msingi Kitomanga, Musa Mpwapwa, anakiri kupokea Sh milioji 81 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa mapya matatu, matundu vyoo na madawati.

Anasema baada ya kukarabati miundombinu hiyo, hata walimu wamekuwa na hamasa ya kufundisha na wanafunzi wanahudhuria masomo bila shurti.

Naye Mwalimu Mkuu wa Kilwa Masoko, Mwanahamis Njimbwi, anasema amepokea Sh milioni 81 kutoka Wizara ya Elimu ambazo zimemsadia kuboresha miundombinu ya shule.

Tayari programu ya EP4R iliyoanzishwa mwaka 2014 imezaa matunda. Hadi sasa miundombinu chakavu ya shule za msingi  na sekondari 361, ikiwamo vyumba vya madarasa 1,435, mabweni 261, majengo ya utawala 11, mabwalo manne, vyoo 2,832, nyumba za walimu 12, maktaba nne zimekarabaitiwa sambamba na kuweka maji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles