27.1 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

WALIMU WAPAMBANA WANAFUNZI WAFAULU, WAZAZI WAWATAKA WAJAZE MADUDU

Na Derick Milton, Meatu


SHULE ya Msingi Mabambasi inapatikana katika Kitongoji cha Mabambasi, kilichopo Mjini Mhanuzi, Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, mkoani Simiyu.

Shule hii ilianzishwa mwaka 1989, ambapo tangu ianzishwe haina historia ya kufaulisha wanafunzi. Kila mwaka wanafunzi wake wanaohitimu darasa la saba hushika nafasi za mwisho kitaifa.

Mwaka 2015 shule hii ilishika nafasi ya pili kutoka mwisho kitaifa, katika matokeo ya darasa la saba na mwaka 2017 ilikuwa miongoni mwa shule 10 zilizofanya vibaya. Mandhari ya kupendeza ya shule, hayaakisi matokeo.

 

Walimu

Walimu wa shule hii wanataja sababu shule hii kufanya vibaya kuwa ni wazazi kuwataka watoto wao kutoweka majibu sahihi kwenye mitihani ya kuhitimu darasa la saba ili wasifaulu kwenda sekondari.

Mmoja wa walimu wa shule hiyo, Samson Tingo, anasema matokeo yanayopatikana shuleni hapo yanawavunja moyo kwani huwa wanatumia muda mwingi kuwaandaa wanafunzi wao na kuwapa mbinu za ufaulu lakini huishia kushika mikia.

Anasema licha ya kuwapa mbinu za ufaulu, pia hufanya mitihani ya majaribio mara kwa mara ikiwamo mitihani ya ujirani mwema na huwa wanafanya vizuri, lakini unapokuja mtihani wa taifa wanafeli.

“Suala hili linavunja moyo, haiwezekana jitihada zote hizi hazizai matunda, kila siku darasa zima linafeli mtihani wa Taifa na hivyo kusababisha shule kushika nafasi ya mwisho kitaifa.

“Kila mwaka huwa tunawachuja wanafunzi bora, wa kati na wale ambao uwezo wao ni mdogo kabisa. Mfano, kati ya wanafunzi 30 wa darasa la saba, 15 tunakuwa na uhakika kwamba watafaulu lakini baadae hali huwa tofauti.

“Jambo la kushangaza unakuta wale 15 ambao ndiyo huwa wanafanya vizuri darasani, ndiyo hao hao wanaopata alama sifuri kwenye mtihani wa Taifa, ukifuatilia walivyojibu mitihani unakuta wamechora picha, katuni, wanageuza herufi za majibu sahihi tofauti na zinavyotakiwa kuandikwa ili kuondoa maana halisi ya jibu,” anafafanua Mwalimu Tingo.

Naye Mwalimu Shobi Mussa, anasema licha ya kuishi kwenye mazigira magumu ya kukosa nyumba za kuishi, wamekuwa wakijituma na kufanya kazi kwa bidii ili wanafunzi wote wafaulu lakini huwa wanawaangusha.

“Hapa walimu tupo saba ambao tunaishi katika nyumba mbili, wengine wanaishi jikoni, tuliamua walimu wote kukaa shuleni kwa hali ya kubanana ili kuweza kuwafundisha wanafunzi vizuri lakini mwishowe wanafanya vibaya,” anasema Mussa.

Kila mwaka wazazi, walezi, viongozi wa vitongoji na kijiji huwa wanaitwa shuleni kwa ajili ya kujadili suala la wanafunzi kutoweka majibu sahihi kwenye mtihani, lakini hakuna mabadailiko.

 

Chanzo cha kuweka majibu yasiyo sahihi

Asilimia 90 ya wanafunzi wa shule hiyo wanatoka katika vitongoji vya Mabambasi na Mwamasubi, vyenye jumla ya kaya 70 ambavyo idadi kubwa ya watoto huwa wanafeli.

Viongozi wa vitongoji hivyo, kijiji pamoja na wazazi wanakiri kuwa chanzo cha matokeo mabaya shuleni.

Wanakiri kuwataka watoto wao kutoweka majibu sahihi kwenye mtihani wa kuhitimu darasa la saba kwa sababu hakuna mtu aliyesoma akafanikiwa kimaisha.

“Kwanza tangu shule hii ianzishe mwaka 1989 hakuna mwananchi yeyote kutoka kwenye vitongoji hivi (Mabambasi na Mwamasubi) ambaye amefanikiwa kimaisha kutokana na elimu.

“Kwenye kata ya Mwamanimba hakuna shule ya sekondari hivyo, mwanafunzi atatakiwa kutembea umbali wa kilometa 19 kwenda kata jirani ya Mwamalole kufuata shule ya sekondari,” anasema mmoja wa wazazi Milambo Mboje.

Anasema watoto wakifanikiwa kufaulu, watalazimika kutembea umbali mrefu hivyo watachoka, pia njiani watapata vishawishi ambapo matokeo yake ni watoto wa kike kupewa ujauzito, wavulana watajihusisha na uvutaji sigara na bangi, hivyo hawaoni haja ya watoto wao kufaulu.

 

Viongozi wa kijiji na kata.

Charles Manota ni Mtendaji wa kijiji hicho, anasema wananchi wa vitongoji hivyo wanadhani hata watoto wao wakifaulu hakuna faida watakayoipata.

Anasema wanafunzi wa Shule ya Msingi Mwamanimba wanafanya vizuri katika mitihani ya kuhitimu darasa saba kwa sababu wazazi wao wanafahamu umuhimu wa elimu hivyo huwahimiza kupenda kusoma.

Naye Diwani wa kata hiyo, Paul Zabron, anasema sasa hivi wanachofanya ni kuwahimiza wazazi juu ya umuhimu wa watoto kufaulu na kwamba tangu waanze kueleimishwa sasa wanaanza kuelewa.

“Pia kipindi cha mitihani kinapokaribia tunawatenganisha watoto na wazazi wao ili wasionane na kuwashawishi kujaza madudu kwenye mitihani. Tumegundua ukikaribia mtihani ndiyo wanawatisha na kuwataka wajaze ovyo,” anasema Zabron.

Kwa upande wake Kaimu Ofisa ya Elimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Kidando Hinza, anasema shule hiyo imekuwa ikisababisha wilaya kushika nafasi za mwisho kimkoa na kitaifa kwenye mtihani wa taifa darasa la saba.

Anasema kuwa kutokana na hali hiyo, wameweka mikakati ya kuisimamia shule hiyo kila mara ili kuhakikisha wanafaulisha tofauti na ilivyokuwa zamani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles