Na GUSTAPHU HAULE, KIBAHA
WAKALA wa Barabara Mkoa wa Pwani (Tanroads), umepanga kutumia Sh bilioni 25.4 kutoka katika mfuko wa barabara kwa ajili ya matengenezo mbalimbali ya barabara katika bajeti ya mwaka 2019/20 .
Mapendekezo hayo yalitolewa juzi na Meneja wa Tanroads Mkoa wa Pwani, Yudas Msangi,katika kikao cha bodi ya barabara kilichofanyika mjini Kibaha chini ya Mwenyekiti wake Assumpter Mshama ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kibaha.
Akiwasilisha bajeti hiyo, Msangi alisema katika fedha hizo,Sh Shbilioni 10.8 zitatumika katika matengenezo ya barabara kuu zaidi ya kilomita 528, madaraja madogo 84 na daraja kubwa moja na Sh bilioni 14.6 zitatumika katika matengenezo ya barabara za mkoa.
Alisema kwa barabara za mkoa zina urefu wa kilomita 1009 .70 , madaraja madogo 45 na madaraja makubwa manane, zimepangwa kufanyiwa matengenezo kwa kiwango cha changarawe ya kawaida na muda maalumu, matengenezo ya kawaida ya lami na matengenezo ya muda maalum ya lami.
Alisema bajeti hiyo imezingatia uhalisia na mahitaji ya matengenezo ya barabara za Mkoa wa Pwani na kwamba amewaomba wajumbe wa kikao hicho kushirikiana kwa pamoja kuhakikisha mpango huo wa bajeti unafanikiwa kama ilivyopangwa.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Pwani, Ramadhani Maneno, aliitaka Wakala wa Ujenzi Tanzania (Tanroads) na Wakala wa Barabara Vijijini (Tarura), kuhakikisha wanawalipa fidia wananchi ambao maeneo yao yamewekea alama ya kubomoa.
Maneno alitoa mfano barabara ya Makofia –Mlandizi –Mzenga kuwa wananchi wa maeneo hayo wamewekewa alama ya X muda mrefu kwa kuwataka waondoke maeneo hayo kwa kupisha barabara lakini cha ajabu mpaka sasa wananchi hao hawajalipwa fidia.
Naye Mshama alisema suala la barabara ni jambo muhimu kwa sababu bila kuwa na barabara nzuri hakuna maendeleo.
Aliwaomba Tanroads na Tarura kufanyakazi kwa ufanisi kuweza kufikia malengo.