HARARE, ZIMBABWE
POLISI nchini Zimbabwe juzi walimkamata mchungaji aliyedai Rais mkongwe Robert Mugabe, ambaye mwezi ujao atatimiza umri wa miaka 93, atafariki dunia Oktoba mwaka huu.
Kwa mujibu wa wakili Gift Mtisi, mchungaji huyo, Patrick Mugadza, alikamatwa katika Mahakama ya Harare ambako alisomewa mashtaka tofauti ya kuvalia bendera ya taifa na utabiri alioutoa wiki iliyopita kuhusu kifo cha Mugabe.
“Awali alikamatwa kwa kukwaza mamlaka za rais na shtaka hilo lilibadilishwa kuwa kuwatusi watu wa taifa au dini tofauti,” Mtisi aliliambia Shirika la Habari la Ufaransa (AFP).
Wiki iliyopita, Mugadza aliitisha mkutano na wanahabari na kutangaza kuwa Mugabe atakufa Oktoba 17, mwaka huu.
Kumkejeli au kumtabiria Mugabe ni kitu hatari nchini Zimbabwe, ambako sheria imekataza kukwaza mamlaka au kumtusi rais.
Mwaka 2015, Mugadza alikamatwa na kushikiliwa kwa karibu mwezi mmoja baada ya kushikilia bango linalomwambia Mugabe kuwa watu wake wanaumia kwa utawala wake.
Mugabe yu madarakani tangu taifa hili lipate uhuru kutoka kwa ukoloni wa Kiingereza mwaka 1980.