27.5 C
Dar es Salaam
Monday, October 2, 2023

Contact us: [email protected]

WATANZANIA HATUJAFIKIA HATUA YA KUCHOCHEWA NA MAGAZETI

Na HELLEN KIJO BISIMBA


Askari wkitumia gari la washawasha kudhibiti vurugu
Askari wkitumia gari la washawasha kudhibiti vurugu

KILA ninapofundisha somo la haki za binadamu na hasa aina za haki, ninapenda sana kutoa mfano wa haki za kiitikeli.K wa wale wasiojua aina hii ya haki ni zile ambazo watu wanazipata kutoka kwa jamii.

Ni haki zinazofaidiwa na wanajamii husika na hutofautiana toka jamii na jamii, huwa napenda kueleza jinsi ambavyo kwa Watanzania si sawa kabisa kufika dukani na kusema ‘nipe, nataka sabuni’. Kawaida ni ‘naomba, nisaidie’ n.k .

Mtu asipofanya hivyo huonekana kukosea na mara nyingi husahihishwa na hata  kukemewa. Jirani zetu husema kuwa Watanzania ni watu wataratibu sana, wapole, wenye heshima.

Kuna wanaotutania kuwa hata askari wetu huwa wanaomba kumkamata mhalifu. Na ni kweli kuwa nchi yetu ina sifa ya kuwa kisiwa cha amani. Hivi ndivyo tunavyoeleweka  kama Watanzania pamoja na kuwa wapo wengine ambao hawatoi haki hii kwa wenzao kwa kuwa na tabia za kuongea tofauti na Watanzania kwa ujumla.

Kwanini ninakumbuka hili somo na haki ya Watanzania? Wiki iliyopita nimekutana na matukio kadhaa yaliyonifanya nijaribu kujiuliza hivi kuna nini kimebadilika kwa Watanzania?

Mojawapo ni pale nilipomsikia rais kupitia vyombo vya habari akisema kuwa kuna magazeti mawili  yanaandika habari za uchochezi na kwa hali hiyo, Serikali yake ya kutumbua majipu itayatumbua.

Niliposikia haya, nilifikiria sana ni kwa vipi magazeti haya yanafanya uchochezi na yanamchochea nani? Siku rais anavyoongea hayo nilitoka kuwasiliana na chombo kimojawapo cha habari ambapo Kituo chetu cha Sheria na Haki za Binadamu huwa tuna kipindi tulicholipia ambapo huwa na mada mbalimbali tunazowasilisha.

Kipindi cha mwisho wa mwaka kilipaswa kutathmini hali ya haki za binadamu nchini, lakini kwa hali ya kustaajabisha chombo hicho cha habari kiligoma kutupa fursa ya kurusha kipindi hicho.

Walipata hofu kuwa katika kuzungumzia hali ya haki za binadamu, tutawagusa wakubwa na tunaweza kuwasababishia kupewa adhabu ikiwemo kufutwa. Nilishangaa sana hasa nilipowasihi watupatie majibu hayo kwa maandishi na wakasema hawatathubutu kufanya hivyo.

Hii maana yake ni nini? Ni hofu. Na je iwapo chombo cha habari kinakuwa na hofu kiasi hiki, Watanzania wa kawaida wako katika hali gani?

Siku hiyo pia nikiwa katika maongezi na vijana fulani sehemu, wakawa wanalalamika kuwa wanadhani kura zao ziliibwa, nikawaambia kama kura ziliibwa mbona wasingeandamana kuonyesha kutoridhika?

Hawa waliniangalia kwa  mshangao wakasema: “Kwani hapa ni  Marekani unataka  tupate mkong’oto ambao hatutausahau maishani?”

Lakini pia nikakumbuka jinsi huko nyuma palivyokuwa na maandamano mbalimbali nchini ya kisiasa na hata ya mashirika yasiyo ya kiserikali.

Hivi sasa mengi ya maaandamano hayo yamekatazwa na wahusika wameridhika na zuio na wanaendelea na maisha kama kawaida. Ukijiuliza hivi walipotaka kuandamana hapakuwa na hoja?

Kama kulikuwa na hoja, kwanini wameridhika na kukaa kimya? Kuna majibu kadhaa huenda ni kwa vile walitishwa wakatishika au wameamua kuwa waungwana kama ilivyo tabia ya Watanzania na kuisikiliza dola.

Hapa ndipo ninapofikia kusema kuwa Mheshimiwa Rais hana sababu ya kufungia magazeti kwa uchochezi kwani wa kuchochewa hawapo. Watanzania kwa jinsi tulivyo hatuchocheki ni kama kuni mbichi.

Huwezi kabisa kuwalinganisha Watanzania na Wanyarwanda au hiyo nchi nyingine aliyoitaja. Watanzania kwa haiba ni wapole lakini pia ni waoga sana. Na pia Watanzania nikiwemo mimi ni wepesi sana kukubali yaishe.

Haya magazeti yanayosemekana ni ya kichochezi, iwapo kweli yana uchochezi basi ungekuta tumeshachochewa na tumeshalipuka.

Hivi wangekuwa wanaweza kuchochewa   iweje pawepo na mizengwe katika chaguzi mbalimbali za mameya wawe kimya tu? Iweje wachangie wahanga wa tetemeko na  michango hiyo isemekane si ya wahanga ni ya miundombinu ya Serikali nao waone ni sawa tu au waamue tu kunyamaza na kunung’unikia chini chini pamoja na kujua walitoa michango kwa ajili ya wale watu na si vitu?

Hawa ni Watanzania ambao wanapewa maneno yanayoweza kuwa ya kuwaudhi lakini wanacheka na kupiga makofi na hata wakiambiwa baada ya hapo Oyeee!!!! wanaitikia kwa furaha kuu oyeeeee!!!.

Na nikisema hivi huenda mtaanza kusema ninawachochea. Sina wasiwasi kwa vile najua hakuna Mtanzania atakayeweza kuchochewa hata kama maneno haya yatatafsiriwa kuwa uchochezi.

Nilisoma mahali fulani kuwa kuna utafiti umefanyika na ikasemekana kuwa Watanzania ni watu wanafiki au waongo, wanaongoza nadhani Afrika.

Nikaona wengine wakipinga na kusema huo utafiti si wa kweli. Huenda kuna ukweli kiasi. Makamu wa Rais alieleza jinsi watu  katika chama chake wanavyoongea naye masuala pembezoni lakini kwenye vikao wanakuwa kimya.

Mimi nina uzoefu wa watu wanaotoa taarifa  za kuonewa au kutendewa visivyo, kisha wanasema ‘usinitaje’. Lakini katika ngazi ya taifa, nimeona kuna  hali ya watu kutokuwa tayari kuwashauri viongozi katika masuala mbalimbali.

Wengine wanasema ‘sijipendi?’ Ati wanaogopa kutumbuliwa. Sasa watu wa aina hii kweli unadhani watachochewa na nani. Vyombo vya habari kwa kweli vina uwezo mkubwa wa kuweza kuleta uchochezi lakini si kwa Watanzania.

Vyombo vyenyewe pia vingi havina huo ubavu. Ninakumbuka mwaka 2012 wakati wa mgomo wa madaktari, rais aliyekuwa madarakani hakupendezwa na wanaharakati waliokuwa wakiitaka Serikali iongee na madaktari kumaliza mgomo.

Na kwa hiyo, alihoji hao ni watetezi gani wa haki wakati wanaona ni sawa tu haki ya kuishi kuingiliwa na kupotezwa na mgomo huo. Rais alipomaliza kuhutubia kabla hata dakika haijaisha, nilipata simu nyingi kutoka kwa vyombo vya habari mbalimbali wakitaka kujua tunasemaje baada ya rais kutoa kauli hiyo?

Lakini mwaka jana rais aliyepo madarakani, alisema kuwa wanaharakati wa haki za binadamu wanaohoji utumbuliwaji wa majipu wa mafisadi na wao ni majipu wanastahili kutumbuliwa.

Sikusikia na hadi leo sijamsikia mwandishi wa habari aliyenihoji kuwa ninasemaje katika hilo? Maana yake ni nini? Ama wameona si hoja au wamekosa uthubutu.

Mimi ningemshauri rais wetu mpendwa aache tu magazeti yafanye kazi zake kwa njia wanazoona zinafaa, kama wasiwasi ni kuwa yanafanya uchochezi kwa sababu mchochewaji hayupo kabisa labda kama yanatumia lugha chafu, yasahihishwe ili yatumie lugha ya staha.

Lakini kama yanaandika mambo ambayo hayafurahishi kwa wengine, basi wasamehewe tu kwa vile tusitegemee kuwa wote tutakuwa tunafurahishwa na yote pamoja na itikeli yetu kuwa ya kufanana kama Watanzania.

Stahamala za kisiasa na kijamii ni nguzo kubwa sana ya kidemokrasia, ndio maana nilimfurahia sana rais alivyopokea vibonzo vinavyomchora. Vivyo hivyo kwa wengine wote tuendeleze Utanzania wetu kwa kuweza kustahimiliana katika hali yetu hii ya amani.

Na upande mwingine, pia tuhakikishe misingi yote mikuu ya demokrasia inafanyiwa kazi, kwani yaliyotokea nchi jirani si hasa vyombo vya habari bali kulikuwa na mambo yaliyokuwa mioyoni mwa watu hao ya muda mrefu.

Vyombo vile vikawa kama kiberiti kilichopitishwa jirani na petroli. Hapa hatujawa na petroli bado, ila tusipoangalia tutaitengeneza na hapo ndipo itatubidi tuogope moto kwa njia ya vyombo vya habari. Mungu ibariki Tanzania  na watu wake.

Mwandishi ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles