Na Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital
Mashindano ya Taifa Klabu ya Kuogelea yameanza leo Aprili 20,2024, huku waogeleaji kutoka klabu mbalimbali wakionekana kuchuana vikali kwenye bwawa la kuogelea la Shule ya Kimataifa ya Tanganyika(IST), Masaki jijini Dar es Salaam.
Michuano inayotarajiwa kumalizika kesho Aprili 21,2024 inashirikisha jumla ya klabu 11 za Tanzania na mbili zikitokea nchini Kenya.
Akizungumzia  mwanzo wa mashindano hayo, Mwenyekiti wa Chama cha Kuogelea Tanzania(TSA),David Mwasyoge, amesema mashindano hayo yana ushindani mkubwa kwa sababu washiriki  ni wale waliofikia vigezo  vya dunia.
“Mashindano haya klabu zimepungua  na hata washiriki ni wachache kwa sababu yana ushindani wa hali ya juu na  ilikuwa ili uweze kushiriki lazima ufikie vigezo vya dunia,”amesema.
Ameeleza kuwa mikakati ya chama ni kuhakikisha  vijana wengi wa Kitanzania wanashiriki katika mchezo wa kuogelea na kuondoa dhana kuwa mchezo huo ni wa matajiri.
“Tanzania ina vipaji vingi vya kuogela na tumegundua watoto wengi wanapenda maji, sababu ukiangalia kwenye sherehe nyingi wazazi wanawapeleka watoto wao kwenda kuogelea, kwa hiyo lengo letu ni kuwapa mafunzo,” amesema.
Kwa upande wake muogeleaji  Crissa Dillip,  amesema mashindano ni magumu kutokana na ushindani uliopo lakini anaamini atafanya vizuri na kuwa miongoni mwa wachezaji bora wa michuano hiyo.