MWENYE macho haambiwi tazama na anayeshindwa kushukru kwa jambo dogo hata akifanyiwa jambo kubwa kwake ni upuuzi.
Ni ukweli usiopingika ikiwa bado siku kumi kutimia mwaka mmoja tangu kuapishwa Rais Magufuli, amefanya mambo makubwa kiasi kwamba ukipingana na hilo utaonekana mwendawazimu.
Novemba 6, 2015 siku moja baada ya kuapishwa ilikuwa ni mwanzo wa mapambano kwake, kwani aliweza kufanya ziara ya kushtukiza katika taasisi muhimu ya Wizara ya Fedha na kukuta madudu kadhaa.
Kushtukiza haikuwa nguvu ya soda kwani Novemba 9, aliamua kuibukia katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na kukuta vichekesho kwamba vipimo vya CT-Scan na MRI havifanyi kazi huku hospitali za binafsi vikiwa hai.
Rais akiwa amechukizwa na uzembe katika hospitali hiyo, aliamua kumuondoa Kaimu Mkurugezi Dk. Hussein Kindato huku akiamuru vipimo hivyo kutengenezwa mara moja.
Hatua ya kumuondoa Dk. Kindato ilikuwa ni mwendelezo wa utumbuaji kwa wazembe, maana baada ya hapo tumeshuhudia vigogo wa Mamlaka ya Bandari, mapato, Mkurugenzi Vitambulisho vya Taifa, TAKUKURU, Uhamiaji na TRL wakiwekwa kapuni.
Ni kiongozi pekee amezuia shamrashamra za Sikukuu ya Uhuru, Muungano, Mwenge, hafla za kuapishwa viongozi bila kusahau safari bubu nje ya nchi kama njia ya kubana matumizi.
Ubunifu wa kiongozi huyu ndio umesababisha kulivalia njuga suala la watumishi hewa ambao walikuwa kitega uchumi cha wasaliti wa nchi.
Amejitahidi kutimiza ahadi ya elimu bure huku akitengeneza madawati kwa shule za Serikali ili kuondoa kero ya muda mrefu.
Kama Baba wa Taifa, haiba ya Rais Magufuli inaonesha kuwa anachukia sana rushwa na ufisadi kwani ameamua kujenga mahakama rasmi kushughulikia vitendo hivyo.
Rais huyu haoni aibu kuwapoteza aliowateua kwani tumeshuhudia baadhi ya wakurugenzi, makatibu tawala na wakuu wa mikoa wakitenguliwa baada ya kugundulika udhaifu.
hayo yakiwa ni machache kati ya mengi aliyoyafanya Rais Magufuli,nlakini kiongozi huyu anasutwa na wengi kuwa anaizika demokrasia kama njia mojawapo ya kukwepa kukosolewa.
Uchaguzi wenye kutia shaka huko Zanzibar huku Rais wa Muungano akitoa kauli chungu badala ya asali ili kujenga mwafaka ni ufa mkubwa.
Serikali kuzuia kurushwa ‘Live’ mijadala ya Bunge kama ilivyozoeleka inatafsiriwa ni kuwapumbaza wananchi ili wasielewe udhaifu wa watawala.
Wanaokamatwa kwa kuhisiwa kumtukana Rais inaashiria woga, kwani ‘‘Mkubwa ni jaa’’ hivyo kusutwa na kunenewa mabaya ni sehemu ya kupima uvumilivu katika uongozi.
Vyama vya upinzani kuzuiwa kuendesha mikutano yao kwa kisingizio cha kufanya kazi ni uonevu na kuwanyima wananchi wasifichue mambo ambayo wanaona bado hayajakaa sawa.
Wengi wanaamini endapo patakuwapo uhuru wa kujieleza ni rahisi kuelewa hisia za watawaliwa na kufichua maovu ambayo yanaweza kufanywa na wasaidizi wa Rais kwa siri na kwa maarifa ya hali ya juu ukizingatia Rais hana utani.
Kuna ukosefu wa dawa hospitalini, kuna changamoto kwenye elimu bure maana yapo manung’uniko kuwa pesa inayotolewa haitoshi. Hayo yatafichuliwa endapo wananchi watakuwa huru kutoa maoni.
Hata hivyo ‘‘Mvumilivu hula mbivu na subira huvuta heri’’ kwani pamoja na upungufu uliopo, bado wananchi wana imani kubwa na Rais wao japo watumishi wa Serikali ndio wanaonekana kukata tamaa na kuhisi kuwa ahadi alizowaahidi ni za ujenzi wa ghorofa angani.