23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Adhabu ya kifo: Ililetwa na wageni, wameiacha

kitanziMWEZI huu ulikuwa na masuala mengi ya kuangalia katika anga na medani za Haki za Binadamu na hata kisiasa moja kwa moja. Oktoba 10 mwaka huu ilikuwa ni Siku ya  Kimataifa ya kupinga adhabu ya kifo wakati Oktoba 11 ilikuwa ni siku ya mtoto wa kike kimataifa.

Kitaifa tulikuwa na siku ya kumbukizi la Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere. Kila siku ilikuwa na umuhimu wake na kila moja iliadhimishwa kwa aina yake na makundi mbalimbali.

Hii siku ya kupinga Hukumu ya Kifo iliadhimishwa kimataifa ikiwa na kauli mbiu kuwa adhabu hii ni nyenzo ya magaidi. Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kiliadhimisha siku hii kwa njia tofauti mwaka huu.

Kwanza ilikuwa ni kwa kutoa tamko kwa vyombo vya habari na kujadili adhabu hii. Pili ilikuwa ni kwa kuandaa kongamano lililohusisha wadau mbalimbali wakiwamo viongozi wa kidini, viongozi wa kimila na  watendaji wa Serikali pamoja na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.

Suala la kupinga adhabu ya kifo halikuanza leo na hivyo kampeni hii inavyoendelea kuna mambo mengi sana ya kujifunza ili kuzidi kuwasaidia wale ambao bado hawajaona ubaya wa adhabu hii.

Katika kongamano lililofanyika  Oktoba 20, mwaka, masuala yaliyojitokeza ambayo ni vyema tukayajadili hapa. Wajumbe wa kongamano hilo waliopata karibu watu 70 au zaidi walitoa hoja ambazo nyingine zilikuwa ngeni.

Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu, Bahame Tom Nyanduga alitoa historia na chimbuko la adhabu hii ya kikatili hapa nchini. Alionyesha kuwa adhabu hii ililetwa na wakoloni wa Kijerumani mwaka 1886 kwa manufaa yao ya kututawala.

Adhabu hii ya kifo ikapokelewa na Waingereza ambao mwaka 1945 waliitungia sheria kwa kuweka kipengele katika sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 ya sheria. Serikali ya uhuru nayo iliendelea na sheria hii hadi sasa. Alizungumzia jinsi adhabu hii isivyokidhi vigezo vya kuitwa adhabu kwani nia ya kutoa ni kurekebisha na kutoa fundisho kwa wengine.

Adhabu hii haiwezi kumrekebisha mtu ikishatekelezwa na pia ushahidi uliopo unaonyesha kuwa haijasaidia kupunguza  kosa hilo.

Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini, yeye aliwapa moyo wale wanaoipinga adhabu hii kwa kusema kuwa vita wanayoipigania ni ya kushinda kwani hadi sasa nchi 141 ambazo ni zaidi ya 32 ya nchi zote duniani, zimeshaachana na adhabu hii.

Na alisema nchi zote wanachama wa Nchi za Ulaya wameacha kabisa adhabu hii ya kifo na nchi yoyote inayotaka kuwa mwanachama lazima iwe haina adhabu ya kifo katika vitabu vyake vya sheria.

Alisema pia zipo nchi karibu 20 za Afrika ambazo zimeachana na adhabu hii ya kifo. Haya yalitupa sababu ya kujitafakarisha kuwa iwapo nchi hizi za Ulaya ambazo ndizo zilileta adhabu hii hapa kwetu na wao wameiacha kwanini nchi zetu za Afrika bado zinainga’nga’nia?

Kongamano lilipata uzoefu kutoka kwa viongozi wa kimila mmoja akiwa ni wa kabila la Mkoa wa Kagera, Chifu wa Wahaya na mwingine akitokea katika kabila la Kimasai (Maa). Viongozi wote hawa walionyesha kuwa katika jamii za kimila  makosa ya mauaji yalikuwapo ila waliokosa walishughulikiwa tofauti kabisa na ilivyo sasa. Kwa kabila la Wahaya mtu aliyeuawa na mtu mwingine alitengwa na hivyo hakuweza kushiriki shughuli za umma.

Hata kula ilibidi mtumishi wa Chifu ndio ampelekee mahitaji yake. Baada ya kipindi cha kutengwa kisha alirejeshwa katika jamii na kusaidiwa kurudi katika hali ya  kiusalama zaidi.

Kwa Wamasai wao walikuwa wanakaa jamii mbili husika, wale waliofiwa na ndugu kutokana na mauaji na wale ambao ndugu yao ndio aliua. Jamii hizi huwa na kazi kubwa ya kutafuta suluhu kati ya jamaa hizo husika.

Pamoja na suluhu yule mkosaji hupelekwa katika eneo la Kichuguu na kutakiwa kutubu kosa lake. Baada ya hapo basi muuaji hutozwa faini ya ng’ombe 49 iwapo muuaji alikuwa mwanaume na 39 iwapo muuaji alikuwa mwanamke.

Kisha yule muuaji hufanyiwa utakaso ili aweze kurejea katika jamii na kuendelea kuwa mtu mwema. Hawa viongozi wa kimila walisisitiza kuwa nia kubwa ilikuwa ni kupata suluhu na kutoa fidia na si kuwafungia watuhumiwa au kuwaua.

Viongozi wa dini walitofautiana ambapo wapo waliosema kumuua muuaji ni haki yake na hii ni amri ya Mungu kama ilivyoshushwa mwaka 610 AD.  Upande mwingine mwakilishi walisema adhabu ya kuua haikubaliki na akatoa mfano wa mtu wa kwanza kuua katika maandiko akiwa ni  Kaini aliyemuua mdogo wake lakini Mungu hakumuua ila alimlinda  ili asiuawe na watu wengine.

Katika yote haya tuligundua kuwa katika  kongamano lile walikuwapo watu wengi waliokuwa wanakubaliana kuwa adhabu ya kifo haifai na ni ya kutweza utu wa mtu na hivyo basi inabidi ifutwe kama ilivyofutwa katika nchi nyingine duniani na Afrika.

Hata hivyo walikuwapo wachache walioona adhabu hii iendelee. Suluhisho halikuweza kupatikana moja kwa moja ila ukweli kuwa adhabu ya  kifo haipaswi kutumika ulikubalika. Iwapo walioileta wameiacha sisi tunasubiri nini?

Hata hivyo zipo sababu nyingine nyingi zinazoonesha umuhimu wa kuachana na adhabu hii. Hii ni adhabu inayotweza utu wa mtu. Na kwa vile utu na uhai ni vya msingi sana, ili mtu awe mtu basi ni lazima awe hai. Serikali ikimuua muuaji inarudia kosa alilolifanya. Adhabu ya kifo ikikosewa hairekebiki.

Kwa mifumo ya sheria tuliyonayo ni rahisi kabisa kukosea na hivyo mtu asiyehusika kabisa akauawa na pasiwe na kitu cha kufanya. Vile vile adhabu hii ni ya kibaguzi kwani wanaopatikana na hatia mara nyingi ni wale wasio na uwezo wa kuweka mawakili. Pia haijawahi kuthibitika kuwa imesaidia kupunguza vitendo vya mauaji kwa kukusudia.

Haya pamoja na mengine mengi yalijadiliwa katika kongamano mwaka huu na swali kubwa limebaki iweje walioileta adhabu hii waiache na sisi tulioletewa tuikumbatie wakati tuna njia zetu mbadala za kushughulikia mauaji?

Kwanini tusijifunze toka katika mila na tamaduni zetu kuona njia ipi tunaweza kuifuata kama Taifa, bila kuruhusu wauaji waendelee kuuawa bila kupata fundisho la maisha wakati huo huo tukileta suluhu katika jamii?  Serikali ione sababu ya kufuta adhabu hii katika sheria zetu na iache kutunga sheria zinazoongeza adhabu hii .

Mwandishi ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles