26.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Mafanikio ya Rais Magufuli  ndani ya  demokrasia tata

magufulliMWENYE macho haambiwi tazama na  anayeshindwa kushukru kwa jambo dogo hata akifanyiwa jambo kubwa kwake  ni upuuzi.

Ni ukweli usiopingika ikiwa bado siku kumi  kutimia mwaka mmoja tangu kuapishwa  Rais Magufuli, amefanya mambo makubwa  kiasi kwamba  ukipingana na hilo utaonekana  mwendawazimu.

Novemba 6, 2015 siku moja baada ya kuapishwa ilikuwa ni mwanzo  wa mapambano  kwake,  kwani aliweza  kufanya ziara ya kushtukiza katika taasisi muhimu  ya Wizara ya Fedha na  kukuta madudu kadhaa.

Kushtukiza haikuwa  nguvu ya soda kwani Novemba 9, aliamua kuibukia katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na kukuta vichekesho kwamba  vipimo  vya CT-Scan na MRI havifanyi kazi huku hospitali za binafsi  vikiwa  hai.

Rais akiwa amechukizwa na uzembe katika hospitali hiyo,  aliamua kumuondoa Kaimu Mkurugezi Dk. Hussein Kindato huku akiamuru vipimo hivyo kutengenezwa mara moja.

Hatua ya kumuondoa Dk. Kindato ilikuwa ni  mwendelezo  wa utumbuaji kwa wazembe,  maana baada ya hapo tumeshuhudia vigogo wa Mamlaka ya Bandari, mapato, Mkurugenzi  Vitambulisho vya Taifa,  TAKUKURU, Uhamiaji na TRL  wakiwekwa kapuni.

Ni kiongozi pekee amezuia shamrashamra za Sikukuu  ya Uhuru, Muungano,  Mwenge, hafla za kuapishwa viongozi bila kusahau safari bubu  nje ya nchi kama njia ya kubana matumizi.

Ubunifu wa kiongozi huyu ndio umesababisha kulivalia njuga suala la watumishi hewa ambao walikuwa kitega uchumi cha wasaliti wa nchi.

Amejitahidi kutimiza ahadi ya elimu bure  huku  akitengeneza madawati kwa shule za Serikali ili kuondoa kero ya muda mrefu.

Kama  Baba wa Taifa,  haiba ya Rais Magufuli inaonesha kuwa anachukia sana rushwa na ufisadi kwani ameamua kujenga mahakama rasmi kushughulikia vitendo hivyo.

Rais huyu haoni aibu kuwapoteza aliowateua kwani tumeshuhudia baadhi ya wakurugenzi, makatibu tawala na wakuu wa mikoa wakitenguliwa baada ya kugundulika udhaifu.

hayo yakiwa ni machache kati ya mengi aliyoyafanya Rais Magufuli,nlakini kiongozi huyu anasutwa na wengi kuwa anaizika demokrasia kama njia mojawapo ya kukwepa kukosolewa.

Uchaguzi wenye kutia shaka huko Zanzibar huku Rais wa Muungano  akitoa kauli chungu badala ya asali ili kujenga mwafaka ni ufa mkubwa.

Serikali  kuzuia kurushwa ‘Live’ mijadala ya Bunge kama ilivyozoeleka inatafsiriwa ni kuwapumbaza wananchi ili wasielewe udhaifu wa watawala.

Wanaokamatwa kwa kuhisiwa kumtukana Rais inaashiria  woga,  kwani ‘‘Mkubwa ni jaa’’  hivyo kusutwa na kunenewa mabaya ni sehemu ya kupima uvumilivu katika uongozi.

Vyama vya upinzani kuzuiwa kuendesha mikutano yao kwa kisingizio cha kufanya kazi ni uonevu na kuwanyima wananchi wasifichue mambo ambayo wanaona bado hayajakaa sawa.

Wengi wanaamini endapo patakuwapo uhuru wa kujieleza ni rahisi kuelewa hisia za watawaliwa  na kufichua maovu ambayo yanaweza kufanywa na wasaidizi wa Rais kwa siri na kwa maarifa ya hali ya juu ukizingatia Rais hana utani.

Kuna ukosefu wa dawa hospitalini, kuna changamoto kwenye elimu bure maana yapo manung’uniko kuwa pesa inayotolewa haitoshi.  Hayo yatafichuliwa endapo wananchi watakuwa huru kutoa maoni.

Hata hivyo ‘‘Mvumilivu hula mbivu na subira huvuta heri’’ kwani  pamoja na upungufu uliopo,  bado   wananchi  wana imani kubwa na Rais wao japo watumishi wa Serikali ndio wanaonekana kukata tamaa na  kuhisi kuwa ahadi alizowaahidi  ni za ujenzi wa ghorofa angani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles