30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, May 23, 2024

Contact us: [email protected]

Hotuba kali aliyowahi kuitoa Kikwete-1

jakaya-kikwete-3NA MICHAEL MAURUS

KILELE cha mbio za Mwenge wa Uhuru 2016, kilifikiwa mkoani Simiyu ambapo sherehe za kuuzima mwenge huo zilifanyika Ijumaa iliyopita mkoani humo.

Kwa kufahamu madhumuni ya mbio hizo, leo tumeona ni vema tukawaletea moja ya hotuba za kukumbukwa zilizotolewa wakati wa kilele cha mbio hizo mwaka 2014 mkoani Tabora ambapo mgeni rasmi, alikuwa ni aliyekuwa Rais wa Tanzania wakati huo, Jakaya Kikwete.

Hebu tupate sehemu ya maneno ya Rais huyo mstaafu wakati akihitimisha mbio za mwenge huo.

Ndugu Wananchi;
Kama mjuavyo, katika sherehe hizi pia tunakumbuka tarehe na siku kama ya leo mwaka 1999 ambapo mpendwa wetu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alitutoka hapa duniani.  Ilikuwa siku ya majonzi na simanzi kubwa.

Leo, hata hivyo siyo siku ya kuomboleza, bali ni siku ya kusherehekea maisha ya kiongozi wetu mpendwa asiyekuwa na mfano wake na muasisi wa taifa letu lililo huru la Tanganyika, Desemba, 1961 na wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Aprili 26, 1964 kwa kushirikiana na Mzee Abeid Amani Karume.

Katika kipindi cha uongozi wake na uhai wake Mwalimu aliifanyia nchi yetu mema mengi ambayo daima hayatasahaulika.  Hivyo basi, siku kama ya leo ni ya kukumbuka kazi zake nzuri pamoja na mambo mengi mazuri aliyotuachia kama urithi.  Ni siku ya kutafakari na kuona namna gani tutayadumisha na kuyaendeleza.

Sherehe za mwaka huu ni spesheli kweli kweli, kwani zinafanyika siku chache tu baada ya Bunge Maalum la Katiba kukamilisha kazi yake na kukabidhi Katiba Inayopendekezwa.  Katiba hiyo ambayo imepatikana chini ya uongozi wa mwana Tabora, mashuhuri, Samwel Sitta imesisitiza ubora na kuendelea kwa Muungano wa Serikali Mbili alizoasisi Mwalimu Julius Nyerere akiwa na Mzee Abeid Amani Karume.

Bila ya shaka mtakumbuka jinsi Mwalimu alivyoupigania muundo huo kwa nguvu zake zote wakati wa uhai wake.  Hatuna budi kulipongeza Bunge Maalum la Katiba kwa uamuzi wake wa busara ambao unamuenzi kwa dhati Mwalimu Julius Nyerere na kudumisha urithi wake mkuu kwetu ambayo ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.  Sijui tungesema nini katika Sherehe za mwaka huu kama ndiyo tungekuwa na Katiba Inayopendekezwa yenye muundo wa Serikali Tatu?

Mwenge na Taifa Letu
Ndugu Wananchi;
Mwenge wa Uhuru ni moja ya alama muhimu ya umoja wa nchi yetu na utaifa wetu.  Mwenge umebeba falsafa kubwa ndani yake kuhusu nchi yetu na uhusiano wake na watu wengine duniani hasa wanyonge wenye dhiki wasiokuwa na amani.  Wakati wa harakati za kudai Uhuru wa Tanganyika kutoka kwa Wakoloni wa Kiingereza Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema “Sisi tunataka kuwasha Mwenge na kuuweka juu ya mlima Kilimanjaro, umulike hata nje ya mipaka yetu, ulete tumaini pale ambapo hakuna matumaini, upendo mahali palipo na chuki na heshima palipojaa dharau”.

Dhamira hii ilitimizwa tarehe 9 Desemba, 1961 siku Tanganyika ilipopata Uhuru.  Pamoja na kupandisha  bendera ya taifa huru la Tanganyika kwenye Kilele cha Mlima Kilimanjaro naMwenge wa Uhuru uliwashwa.
Miaka michache baadaye utaratibu wa kukimbiza Mwenge ulianza na kuendelea mpaka sasa.  Mwenge wa Uhuru umeendelea kumulika nchi nzima ukipita katika mitaa, vijiji, shehia na majimbo, wilaya na mikoa ukieneza ujumbe wa udugu, umoja, upendo, amani na mshikamano miongoni mwa Watanzania.  Aidha, Mwenge umeendelea kuwakumbusha Watanzania wajibu wa kufanya kazi kwa bidii na maarifa ili kujiletea maendeleo yao na ya nchi yetu.  Pia wapige vita maovu nchini.

Kwa kuzingatia dhima nyingine ya Mwenge wa Uhuru, nchi yetu na sisi Watanzania tumejitolea kwa hali na mali kusaidia ndugu zetu Barani Afrika waliokuwa wanatawaliwa kujikomboa kutoka kwenye makucha ya wakoloni na wabaguzi wa rangi.

Ni fahari kwetu kwamba wananchi wa Msumbiji, Zimbabwe, Angola, Namibia na Afrika Kusini wamepata ukombozi na uhuru wao na sisi tumetoa mchango muhimu.  Ni jambo la faraja kubwa kwamba nchi yetu imeweza kuwapatia hifadhi ndugu zetu wa nchi jirani na hata mbali wakati maisha yao yalipokuwa hatarini kwa sababu ya kukosekana kwa amani au kwa kukimbia mateso ya uongozi wa kikatili na kidikteta.  Ndugu zetu wa Kongo, Burundi, Rwanda, Uganda, Kenya na Comoro wanajua ukweli huo.  Na, kwa Uganda tuliwasaidia kuling’oa dikteta Idd Amin na Comoro tumewasaidia kuunganisha tena nchi yao.

Hivi karibuni ndugu zetu wa Sudani Kusini waliniomba tuwasaidie kupatanisha makundi makuu yanayohasimiana katika Chama chao kikuu cha SPLM.  Nimekubali, hivyo tutaanzisha mchakato huo tuone tutafika nao wapi.

Wiki ya Vijana 

Ndugu Wananchi;
Kama sehemu ya sherehe hizi, jana nilitembelea Kijiji cha Mfano cha Vijana katika wilaya ya Sikonge.  Nimefurahishwa sana na juhudi zifanywazo na vijana za kujiletea maendeleo.  Nimevutiwa na miradi mbalimbali wanayoitekeleza pale ikiwemo ya kufuga nyuki na kuvuna mazao yatokanayo na nyuki, ufugaji wa kuku na ng’ombe wa maziwa, ushonaji nguo na viatu.  Halikadhalika, shughuli za kilimo na ujenzi wa nyumba bora.  Nimewashauri viongozi wa Wilaya, Mkoa na Wizara waangalie uwezekano wa kuwafanya vijana hao kuwa wakaazi na wamiliki wa eneo hilo la miradi ili kiwe kweli kijiji cha mfano badala ya kuwa mahali pa kupita mithili ya chuo cha mafunzo ya amali.
Baadae nitapata nafasi ya kutembelea mabanda ya maonesho ya kazi wafanyazo vijana na wadau wengine hapa uwanjani.  Maonyesho haya yanathibitisha kwa uwazi fursa zilizopo za kuwaendeleza vijana.  Lililo muhimu kufanya, ni kwa vijana kuwa na upeo mzuri wa ufahamu wa mambo, ubunifu, moyo wa kujituma na kufanya kazi kwa bidii.  Mkifanya hivyo tutaondokana na tatizo la ukosefu wa ajira na umaskini kwa vijana na taifa kwa ujumla.

Ndugu Wananchi;

Kwa kutambua ukweli huu, ndiyo maana Serikali zetu zimeongeza bajeti katika Mifuko ya Maendeleo ya Vijana kupitia Wizara zetu mbili zinazosimamia na kuratibu maendeleo ya vijana.  Shabaha yetu ni kuwawezesha vijana wengi zaidi kupata mikopo na kuwa na mitaji ya kutekeleza miradi yao itakayowawezesha kujiajiri wenyewe na kujipatia kipato. Naikumbusha Wizara inayosimamia na kuratibu Mfuko wa Maendeleo ya Vijana kuhakikisha kwamba fedha za Mfuko huo zinawafikia walengwa na, kwa wakati muafaka.

Kwa upande mwingine nazikumbusha Halmashauri zote za Wilaya na Miji kutekeleza kwa ukamilifu agizo la kutenga asilimia 10 ya mapato yao kwa mwaka kwa ajili ya shughuli za maendeleo ya Vijana na Wanawake.  Ninazo taarifa kuwa baadhi ya Halmashauri zinalitekeleza vizuri agizo hili lakini zipo nyingine ambazo zinasuasua.

Nataka isiwepo hata Halmashauri moja ya kunyooshewa kidole kwa kutokufanya vizuri kwa jambo lenye manufaa kwa vijana wetu kama hili.  Naomba nitumie nafasi hii leo kuzitaka Halmashauri zote kutoa taarifa za mara kwa mara za utekelezaji wa agizo hili.  Taarifa ya kwanza kwa ajili hiyo itolewe mwisho wa mwezi Desemba, 2014, ifuatayo iwe miezi minne baadae na kila baada ya miezi minne.

Usikose nakala yako ya Mtanzania Jumatano ijayo ili kupata mengi mazuri yaliyomo katika hotuba hii ya JK.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles