Na JANETH MUSHI, ARUSHA
KESI mbili za uchochezi zinazomkabili Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), zinatarajia kusikilizwa leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Arusha.
Desemba 21, mwaka jana, kesi hizo zilikwama kusikilizwa baada ya mbunge huyo anayeshikiliwa katika Gereza la Kisongo, kushindwa kufika mahakamani hapo kwa madai kuwa alikuwa anaumwa.
Katika kesi ya kwanza namba 351 ya mwaka jana, Lema na mkewe, Neema Lema, wanakabiliwa na kesi ya uchochezi wakidaiwa kutoa kauli za kashfa dhidi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo.
Kutokana na shauri hilo, watuhumiwa hao leo wanatarajia kusomewa maelezo ya awali ya kesi hiyo.
Katika kesi nyingine namba 352 ya mwaka jana, Lema na mkewe huyo, wanadaiwa kuwahamasisha watu kukusanyika na kufanya maandamano kinyume na sheria.
Katika shauri hilo, upande wa jamhuri utaanza kutoa ushahidi wake leo.
Awali, akisomewa hoja za awali za kesi hiyo, ilidaiwa kuwa, katika tarehe isiyojulikana kati ya Agosti mosi hadi 26, mwaka jana, Lema akiwa mbunge na kiongozi wa Chadema, alirekodi na kusambaza ujumbe mfupi kupitia mtandao wa kijamii uitwao ‘whatsapp’ akihamasisha watu kukusanyika na kufanya maandamano yasiyo na kikomo kuanzia Septemba mosi mwaka jana.
Kesi hizo zilizokuwa zinasikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Agustino Rwizile, Lema alikuwa akiwakilishwa na Wakili Sheck Mfinanga wakati upande wa Jamhuri uliwakilishwa na Wakili Elizabeth Swai na Alice Mtenga.
Leo, Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai mkoani hapa, George Katabazi, ndiye anatarajiwa kuanza kutoa ushahidi wake.
Lema anashikiliwa kwa zaidi ya miezi miwili katika Gereza Kuu la Kisongo baada ya kukamatwa Novemba 2, mwaka jana akiwa nje ya ukumbi wa Bunge mjini Dodoma.
Baada ya hapo, alifikishwa mahakamani Novemba 8, mwaka jana akikabiliwa na mashtaka ya uchochezi dhidi ya Rais Dk. John Magufuli.