22.1 C
Dar es Salaam
Sunday, June 23, 2024

Contact us: [email protected]

Kumbilamoto atuma salamu kwa madiwani, wenyeviti wanaogombana

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Omary Kumbilamoto, amewatolea uvivu madiwani na wenyeviti wanaoendekeza migogoro kwenye maeneo yao kwani wanachelewesha maendeleo ya wananchi.

Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Tabu Shaibu, akimkabidhi cheti cha pongezi Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Amani, Daniel Malagashimba, kutambua mchango wake kwa ajili ya maendeleo ya wananchi. Kulia ni Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Omary Kumbilamoto na Kushoto ni Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Ilala, Mohamed Pazi.

Akizungumza leo Oktoba 29, wakati wa uzinduzi wa ofisi ya Ofisa Mtendaji Mtaa wa Amani iliyopo Kata ya Kipunguni, amesema baadhi ya madiwani na wenyeviti hawaelewani hatua inayoleta ugumu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Ofisi hiyo iliyogharimu Sh milioni 29.2 imejengwa na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Amani, Daniel Malagashimba, kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo.

“Hivi vyeo Mwenyezi Mungu ndiye anayepanga si mwanadamu, niwaombe sana wenyeviti na madiwani muwe wamoja, mfanye kazi kwa pamoja tunamsaidia rais wetu mpendwa lengo na madhumuni kila mmoja aache ‘legacy’…mwisho wa siku historia ndiyo itasema,” amesema Kumbilamoto.

Aidha ameagiza Sh milioni 200 zilizotengwa kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya cha Kata ya Kipunguni ziendelee kuhifadhiwa kwenye akaunti ya jiji ambalo ndilo litahusika kutafuta mkandarasi ili kuepusha migongano ya kimasilahi.

“Fedha zisiletwe kwenye kata zibaki kwenye akaunti ya jiji atafutwe mkandarasi hapa aletwe fundi tu kujenga. Zikija hapa kila mtu atajiona mkubwa matokeo yake kumpata mkandarasi itakuwa shida,” amesema.

Meya huyo amempongeza Malagashimba kwa ujenzi wa ofisi hiyo pamoja mwananchi wa eneo hilo, Dankan Mwaisumo aliyetoa kiwanja.

“Umeacha alama kubwa sana, umeipunguzia mzigo Serikali katika kujenga ofisi au kulipia gharama za kodi…ukiweka umeme nakuletea televisheni kwenye ofisi yako,” amesema Kumbilamoto.

Naye Malagashimba amesema walianza kazi bila kuwa na ofisi na kwamba walifadhiliwa na mmoja wa wananchi aliyewapa vyumba viwili.

“Hii ofisi imepatikana kutokana na biashara yangu ya utalii na kushirikiana na wadau wangu wa maendeleo, sijachangisha mwananchi yeyote. Huduma za barua nazo ni bure na haruhusiwi mtu yeyote kumchangisha mwananchi Sh 2,000,” amesema.

Mwenyekiti huyo pia ameajiri mgambo ambaye anamlipa mwenyewe kuhakikisha ulinzi upo wa kutosha katika mtaa huo.

Aidha amemuomba mkurugenzi wa jiji na wadau wengine kuwasaidia katika ujenzi wa choo cha wananchi ambao tayari yeye amechangia Sh milioni 1 huku wanachama wa Klabu ya Simba tawi la Mkolemba Kipunguni B wakichangia mifuko minne ya saruji.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Tabu Shaibu, ameahidi watakapofanya marekebisho ya bajeti Desemba watatenga fedha kusaidia ujenzi wa choo hicho.

Awali Diwani wa Kata ya Kipunguni, Steven Mushi, amesema kupitia mgawo wa fedha za ujenzi wa madarasa wamepata madarasa manane ambayo ujenzi wake utaanza hivi karibuni.

Kuhusu miundombinu ya barabara amesema barabara ya Moshi Bar – Kwa diwani – Bombambili tayari mkandarasi amepatikana.

“Nimshukuru sana na nimpongeze ndugu yangu Malagashimba haya ndiyo mambo tunayopenda,” amesema Mushi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles