22.9 C
Dar es Salaam
Monday, September 9, 2024

Contact us: [email protected]

Kesi iliyozima nyota ya R. Kelly

HATIMAYE R. Kelly amekutwa na hatia katika kesi ya unyanyasaji wa kingono iliyokuwa ikimkabili staa huyo wa muziki wa R&B nchini Marekani. R. Kelly aliyewahi kutamba na wimbo ‘I Believe I Can Fly’, amekutwa na hatia akitajwa kutumia ustaa wake kuendesha kwa miaka zaidi ya 20 biashara ya ngono iliyodhalilisha wanawake, hasa wasichana wenye umri mdogo.

Udhalilishaji kwa maana gani? Mahakama ilibaini kuwa R, Kelly (jina halisi Robert Sylvester Kelly) aliendesha kwa siri kubwa biashara ya kuuza wanawake, achilia mbali aliofanya nao ngono.

Katika biashara yake hiyo, alisafirisha wanawake kutoka sehemu moja hadi nyingine ndani ya majimbo ya Marekani, lengo likiwa ni kuwapeleka kwa wateja wake.

Mbali ya hilo la kusafirisha wanawake kwa lengo la kuwauza, pia R. Kelly alikutwa na hatia ya kuendesha magenge ya kihalifu akiwatumia zaidi watu wake wa karibu ili kuficha jina lake kubwa kwenye tasnia ya muziki.

Majanga yalianzia wapi? Ni kweli zilikuwapo kashfa nyingi dhidi ya R. Kelly juu ya unyanyaji wa kingono tangu miaka ya 1990. Kumbuka kuhusu Aaliyah, ikielezwa kuwa bibiye huyo alikuwa na umri wa miaka 14 tu wakati anafunga ndoa na R. Kelly.

Vilevile, wafuatiliaji wa maisha ya staa huyo watakuwa hawajasahau tukio la R. Kelly kukamatwa mwaka 2002 baada ya video iliyomuonesha akiwa faragha na binti wa miaka 14 tu.

Hata hivyo, anguko lake kwenye tasnia ya muziki ni pale tu ilipoibuka makala ya ‘Surviving R Kelly’ mwaka 2019, ambayo ndani yake wako wanawake wanaosimulia mwanzo mwisho namna staa huyo alivyowadhalilisha kingono.

Kuanzia kipindi hicho, R. Kelly akawa anahudhuria mahakamani akitokea gerezani na hadi sasa ndiko aliko akisubiri siku ya hukumu.

Waliomkangaa mahakamani Walalamikaji 11, wakiwamo wanawake tisa na wanaume wawili, walisimama kizimbani kwa wiki sita za usikilizaji wa kesi hiyo, wakitoa ushuhuda wa namna nyota huyo alivyokuwa mdhalilishaji.

Mmoja ya wanawake alielezea Mahakama namna R. Kelly alivyomteka, kumtesa na kisha kumbaka. Mwanamke huyo akaongeza kuwa alikumbana na vitisho kutoka kwa staa huyo tangu alipoanika machafu yake hayo.

“Nimeamua kuanza upya maisha yangu, nimeamua kuacha woga na kuanika kila kitu ili nipone maumivu niliyonayo,” amesema aliyejitambulisha Mahakamani kwa jina la Sonja.

Mwingine aliyefika Mahakamani ‘kumkaanga’ R. Kelly ni bibiye Lizette Martinez aliyedai kufurahishwa na namna wanawake wenzake walivyoamua kuanika kila chafu lililofanywa na mwanamuziki huyo.

Kabla ya hao wote, tayari meneja wake wa zamani, Demetrius Smith, alishaanika kila kitu, akisema R. Kelly alimpa Dola 500 (zaidi ya Sh mil. 1 za Tanzania) ili iwe ni rushwa kwa mtumishi wa Serikali aliyetengeneza cheti cha kudanganya umri wa Aaliyah aliyemuona akiwa mdogo.

Mwanasheria akoleza moto Gloria Allred ni mwanasheria aliyekuwa akimwakilisha mmoja ya wanawake waliodai kunyanyaswa kingono na R. Kelly.

Anasemaje juu ya kesi ya staa huyo? “Nimekuwa kwenye kazi hii ya uanasheria kwa miaka 47. Kwa kipindi chote hicho, nimekutana na wanyanyasaji wa kingono wengi lakini Kelly ndiye kiboko zaidi.

” Kauli ya Gloria inatokana na madai kuwa wanawake aliokuwa akiwatumia R. Kelly kwenye biashara ya ngono walipitia mateso makali, ikiwamo kufungiwa ndani, kutopewa chakula kwa wakati, kutokwenda chooni bila ruhusa yake, pia hata kufanyishwa ngono mbele ya kikundi cha watu. Jela miaka mingapi?

R. Kelly amerejea gerezani akisubiri hukumu inayotarajiwa kusomwa ifikapo Mei 4, mwakani.

Kwa mujibu wa makosa hayo, huenda ikawa ni mwisho kumuona staa huyo uraiani, kwamba huenda akakumba na kifungo cha maisha gerezani. Kwa upande mwingine, mwanasheria wake, Deveraux Cannick, amesema R. Kelly amesikitika kusikia amekutwa na hatia na wanajipanga kukata rufaa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles