Bethsheba Wambura, Dar es Salaam
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali (IGP) Simon Sirro amesema, wameimarisha ulinzi nchi nzima.
Akizungumza na Mtanzania Digital leo Juni 21, IGP Sirro amesema suala la kuwako kwa tetesi za shambulio katika eneo la Masaki jijini Dar es Salaam wanalifanyia kazi na amerudia kusisitiza jeshi hilo kuimarisha usalama si tu katika eneo hilo bali nchi nzima.
Katikati ya wiki hii ubalozi wa Marekani nchini ulitoa taarifa ya kuwapo kwa uvumi wa shambulio katika eneo la Masaki, hususani katika hoteli wanazopenda kutembelea watalii na maduka yaliyopo eneo a ufukwe wa Bahari ya Hindi.
“Timu zetu zinafanyia kazi taarifa hizo, lakini siku zote tupo hivyo., kunapokuwa na amani na utulivu siyo kwamba tumekaa au tumelala, kuna hizi timu zetu za ‘Intelligence’, watu wa operesheni na watu wa upelelezi zimesambaa maeneo mbalimbali kuona kitu gani kipo.
“Ndiyo maana tukiona mtu asiye wa kawaida tunamkamata na kumhoji, kwahiyo sisi tunafanya kazi yetu kama kawaida, kazi hiyo inafanyika maeneo yote yenye watu wengi na si Dar es Salaam pekee bali ni Tanzania nzima.
“Ukizungumzia masuala ya ulinzi unazungumzia Tanzania nzima kwa hiyo haya tunafanyia kazi nchi nzima na si Dar es Salaam tu,” IGP Sirro amewaambia waandishi mara baada ya kumaliza mkutano na Makamanda wa Polisi wa Mikoa na Maofisa wa Polisi uliokuwa ukizungumzia ukatili kwa wa watoto na wanawake uliokuwa ukifanyika Masaki, Dar es Saalaam .