27.3 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 17, 2024

Contact us: [email protected]

IGP Sirro tumeimalisha ulinzi nchi nzima

GRACE SHITUNDU Na LEONARD MANG’OHA

-DAR ES SALAAM

MKUU wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali (IGP) Simmon Sirro amesema, wameimarisha ulinzi nchi nzima.

IGP Sirro ambaye amezungumzia suala la kuwako kwa tetesi za shambulio katika eneo la Masaki jijini Dar es Salaam mara mbili juzi na jana alirudia akisisitiza jeshi hilo kuimarisha usalama si tu katika eneo hilo bali nchi nzima. 

Katikati ya wiki hii ubalozi wa Marekani nchini ulitoa taarifa ya kuwapo kwa uvumi wa shambulio katika eneo la Masaki, hususani katika hoteli wanazopenda kutembelea watalii na maduka yaliyopo eneo a ufukwe wa Bahari ya Hindi. 

“Timu zetu zinafanyia kazi taarifa hizo, lakini siku zote tupo hivyo. Kunapokuwa na amani na utulivu siyo kwamba tumekaa au tumelala, kuna hizi timu zetu za Intelligence, watu wa operesheni na watu wa upelelezi zimesambaa maeneo mbalimbali kuona kitu gani kipo.

“Ndiyo maana tukiona mtu asiye wa kawaida tunamkamata na kumhoji. Kwahiyo sisi tunafanya kazi yetu kama kawaida, kazi hiyo inafanyika maeneo yote yenye watu wengi na si Dar es Salaam na Tanzania nzima,” alisema 

“Ukizungumiza masuala ya ulinzi unazungumzia Tanzania nzima  kwa hiyo haya tunafanyia kazi Tanzania nzima na si Dar es Salaam tu,” IGP Sirro aliwaambia waandishi jana mara baada ya kumaliza mkutano na Makamanda wa Polisi wa Mikoa na Maofisa wa Polisi  uliokuwa ukizungumzia ukatili kwa wa watoto na wanawake  uliokuwa ukifanyika Masaki, Dar es Saalaam .

 Jana ubalozi wa Marekani nchini ulisema tahadhari ya kiusalama waliyoitoa ni utekelezaji wa wajibu wao kuwajulisha raia wa Marekani waliopo nje ya nchi yao.

Ufafanuzi huo mpya wa Marekani umekuja baada ya juzi Serikali kumuita na kumuonya Kaimu balozi wa Marekani  nchini, Inmi Patterson aliyewakilishwa na Janine Young  kuacha kutoa taarifa zinazoweza kuhatarisha amani ya nchi.

Katika majibu yake kwa gazeti hili jana lililotaka kufahamu sababu ya tahadhari hiyo kuendelea  kuwepo kwenye tovuti ya ubalozi huo pamoja na  Young kukiri kwamba yalifanyika makosa katika kuzitoa kwani hazikulenga raia wa nchi yao pekee, Mtaalamu wa Mambo ya Habari ambaye ni Msemaji wa Ubalozi wa Marekani Dar es Salaam,  Ben Ellis alisema;

“Ubalozi unao wajibu wa kuwajulisha wanajumuiya ya Ubalozi wa Marekani kuhusu wasiwasi wowote wa kiusalama.

 “Balozi Mdogo alikwenda Wizara ya Mambo ya Nje kwa niaba ya Kaimu Balozi na kuweka bayana wajibu wetu wa kuwajulisha raia wa Marekani waliopo nje ya nchi yao kuhusu wasiwasi wowote wa kiusalama ambao pia tunawajulisha wanajumuiya ya Ubalozi wa Marekani. 

“Tuna uchukulia wajibu wetu huu kwa umakini na umuhimu  mkubwa kama inavyohitajiwa na Sera ya Marekani ya kutokufanya mambo kwa upendeleo au kuegemea upande mmoja.” alisema  Ellis.

Juni 19 mwaka huu Ubalozi wa Marekani nchini, ulichapisha katika tovuti yake tahadhari ya shambuliz ambayo hadi sasa haijaondolewa kwenye tovuti ya ubalozi huo ikieleza  maeneo yanayolengwa kuwa ni pamoja na mahoteli na migahawa ambayo hutembelewa na watalii, ikiwemo eneo maarufu la maduka ya Slipway.

Kutokana na hilo iliwataka wananchi wake kuwa makini katika maeneo hayo na kuchukua tahadhari.

Pamoja na hayo  ubalozi huo ulisema hauna ushahidi wa moja kwa moja wa tishio hilo ama  taarifa za muda gani mashambulizi yatatokea.

Tahadhari hiyo baada ya kusambaa kwa ilileta hofu kwa wananchi hali iliyofanya viongozi mbalimbali kujitokeza na kuwaondoa hofu.

Kutokana na taarifa hiyo, Wizara ya Mambo ya Nje, ilimwita kaimu balozi wa Marekani nchini juzi, Inmi Patterson ambaye aliwakilishwa na Janine Young kutoa ufafanuzi wa taarifa hiyo.

Taarifa iliyotolewa na kitengo cha mawasiliano cha Wizara hiyo ambayo ilichapishwa kwenye vyombo vya habari jana, ilieleza kuwa katika mazungumzo yake na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk. Faraji Kasidi Mnyepe, Young alikiri ubalozi kufanya makosa kutoa taarifa ambazo hazikuwalenga raia wa Marekani pekee, bali raia wote na zaidi wakitambua  kuwa ubalozi hauna mamlaka ya kufanya hivyo  jambo lililosababisha taharuki kwa wananchi na wageni wanaotarajia kuitembelea Tanzania.

Katika hilo, wizara ya mambo ya Nje ilisema imeukumbusha ubalozi wa Marekani umuhimu wa kuzingatia sheria za nchi na taratibu za kidiplomasia zinazokubalika duniani kote katika utoaji taarifa. 

Kabla Wizara haijamwita Kaimu Balozi wa Marekani nchini, suala hilo tayari lilikuwa limekwishazungumzwa na viongozi wengine wa juu takribani watatu.

Viongozi hao ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola na Mkuu IGP Simmon Sirro na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda. 

Kangi Lugola yeye waliwatoa hofu wananchi na kusema kwamba vyombo vya ulinzi vinaendelea na uchunguzi juu ya suala hilo.

“Nataka niwathibitishie Watanzania nchi imeendelea kuwa na amani na usalama na tutahakikisha maisha na mali za wananchi zinalindwa.

“Vyombo vya ulinzi na usalama viko imara, havitikisiki, vimejipanga vizuri kwa jambo au tishio lolote la kiusalama ambalo linaweza kutokea,”alisema Lugola.

Alisema tahadhari hiyo ya kiusalama ni ya kawaida, ambayo Watanzania hawapaswi kuwa na wasiwasi kwani Serikali iko imara.

“Kama wenzetu wameweza kuzipata na tumewasiliana nao kupitia Jeshi la Polisi, niwahakikishie Watanzania wasiwe na hofu wala wasiwasi, nchi yao iko imara, ina usalama wa hali ya juu.

IGP SIRRO

Aidha IGP, Sirro, alikaririwa na vyombo vya habari siku moja baada ya ubalozi wa Marekani kuchapisha taarifa hiyo akisema walishapata fununu za shambulio hilo kabla ubalozi huo haujatoa tahadhari juu ya tukio hilo.

Kwa mujibu wa IGP Sirro, walipata taarifa kuhusiana na tishio hilo tangu Jumanne wiki hii na kwamba timu zao za operesheni na intelijensia zinaifanyia kazi.

Alisema taarifa hiyo inaweza kuwa ya kweli au uongo, lakini wao kama vyombo vya ulinzi huwa hawapuuzi jambo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles