23.6 C
Dar es Salaam
Saturday, May 18, 2024

Contact us: [email protected]

DMDP kujenga kilomita 73 Segerea

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Kilomita 73 za barabara zinatarajiwa kujengwa kwa lami katika awamu ya pili ya Mradi wa Uendelezaji Jiji la Dar es Salaam (DMDP) na kuwaondolea kero wananchi wa Jimbo la Segerea.

Aidha kilomita zingine 30 pamoja na madaraja ya Kavesu na Kwa Mzava yaliyopo Kata za Liwiti yatajengwa kwa mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.

Akizungumza Februari 10,2024 wakati wa ziara ya kukagua barabara na madaraja yanayotorajiwa kujengwa Mhandisi kutoka Ofisi ya Tarura Ilala, Reginald Mashanda, amesema mradi huo utatekelezwa katika kata zote 13 za jimbo hilo.

Mbunge wa Jimbo la Segerea, Bonnah Kamoli (Kushoto), akivuka katika Kivuko cha Kavesu kilichopo Kata ya Liwiti alipofanya ziara kukagua barabara na vivuko vinavyotarajiwa kuanza kujengwa hivi karibuni.

Amesema usanifu katika baadhi ya barabara ikiwemo ya Barakuda – Chang’ombe – Majichumvi na ile ya Tabata – Kisiwani – Majumba Sita umekamilika na wanatarajia zitaanza kujengwa Aprili,2024.

Amesema pia Daraja la Kavesi tayari usanifu umefanyika na kwa sasa wako kwenye hatua ya kupata mkandarasi wa kulijenga ili lipitike wakati wote.

Mhandisi kutoka Ofisi ya Tarura Wilaya ya Ilala, Reginald Mashanda, akizungumza kuhusu barabara na madaraja yanayotarajiwa kujengwa katika Jimbo la Segerea, Dar es Salaam.

“Zile barabara zenye hali mbaya tumeziwekea mikakati ya muda mrefu ya kuzijenga kwa kiwango cha lami na zege kwa kutumia mapato ya ndani. Mikakati ya muda mfupi ikiwemo kuweka vifusi, kuondoa changamoto kwenye maeneo korofi na kwenye njia za daladala kupitisha greda ziweze kupitika,” amesema Injinia Mashanda.

Naye Mbunge wa Segerea, Bonnah Kamoli, amesema jimbo hilo lina barabara nyingi korofi kutokana na jografia iliyopo ya milima na mabonde.

“Serikali imekuwa ikituona kila mara kwa ajili ya kuangalia miundombinu yetu, Ilala ni kubwa lakini jimbo letu linapewa kipaumbele kwa sababu wananchi wanateseka muda mrefu. Barabara na madaraja tunayategemea tunaomba wakandarasi wafanye kazi usiku na mchana na kwa ubora unaotakiwa,” amesema Bonnah.

Kwa upande wao madiwani wa Kata za Bonyokwa, Buguruni, Liwiti na Segerea wakizungumza kwa nyakati tofauti wamesema wanasubiri kwa hamu utekelezaji wa miradi hiyo na kwamba wananchi wameahidi kutoa ushirikiano kuhakikisha hawaikwamishi.

Diwani wa Kata ya Liwiti, Alice Mwangomo, amesema kilio kikubwa katika kata hiyo ni vivuko vya Kavesi na Kwa Mzava kwa sababu wakati wa mvua mawasiliano yamekuwa yakikosekana na kuwa kero kwa wananchi.

“Mbunge ameendelea kutupa ushirikiano mkubwa katika Kata ya Segerea na kwa kiasi kikubwa kero ambayo tumebaki nayo ni miundombinu ya barabara,” amesema Diwani wa Segerea, Robert Manangwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles