Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Watumishi 16 wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) wanaotarajia kustaafu hivi karibuni wameaswa kuwa makini katika kuchagua miradi ya kufanya baada ya kustaafu ili kuepuka uwekezaji ambao utakuwa na changamoto kubwa kwao.
Badala yake watumishi hao wametakiwa kujikita zaidi kwenye uwekezaji ambao hauhitaji mtaji mkubwa kwa wakati mmoja ili kuweza kupima uwekezaji huo endapo una tija.
Wito huo umetolewa leo Jumanne Agosti 31, DIT na Dk. Haphsa Hincha wa Shirika la Tija laTaifa (NIP), wakati akitoa mada inayohusu uwekezaji mzuri baada ya kustaafu kwa watumishi 16 wa DIT wanaokaribia kustaafu.
Mafunzo hayo ya kujiandaa kustaafu na maisha baada ya kustaafu, lengo lake ni kuwasaidia wastaafu kujua namna ya kujiandaa kustaafu, taratibu za kufuata wanapofatilia mafao yao pamoja na namna ya kujua uwekezaji unaofaa baada ya kustaafu ili waweze kuishi maisha yenye staha.
Aidha, wale ambao hawajawahi kufanya kazi ya ujasiriamali kabisa wameshauriwa kujikita zaidi katika uwekezaji ambao una viashiria kidogo vya hasara jambo ambalo litasaidia kuwapa mwanga ni wapi wawekeze zaidi ili kuepuka changamoto zinazoweza kuepukika zikiwemo za kiafya.
Waashiriki wa semina hiyo wameishukuru menejimenti ya DIT kwa kuwapatia mafunzo haya kwani yametoa  mwanga kwao kabla hawajafikia ukomo wao wa utumishi wa umma. Semina hii inaendeshwa kwa siku mbili kwa wastaafu kutoka Kampasi Kuu ya Dar es Salaaam.