25.5 C
Dar es Salaam
Saturday, May 18, 2024

Contact us: [email protected]

Chalamila atoa maagizo ujenzi barabara ya Bonyokwa -Kinyerezi

Na Esther Mnyika,  Mtanzania Digital

Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam,Albert Chalamila amemtaka mkandarasi wa mradi wa barabara ya Kimara , Bonyokwa na Kinyerezi kuhakikisha anajenga  kwa kiwango walichokubaliana kàtika mkataba na kukamilisha kwa wakati.

Pia mradi huo wenye thamani ya  Sh bilion 24.03,  kujenga barabara zenye urefu wa kilomita 8, daraja moja la Kinyerezi,  makalavati  na taa za barabarani

Chalamila ameyasema  Machi 9,2024  jijini Dar es Salaam  wakati wa hafla ya  kumkabidhi mkandarasi barabara hiyo ambayo ilikuwa kilio  cha muda mrefu kwa wakazi wa Bonyokwa.

“Hii barabara imekuwa ni kilio cha muda mrefu kwa wakazi wa eneo hili, tulikuja hapa kipindi mvua zilivyonyesha na wananchi wakatununia lakini ilikuwa ni wajibu wao kufanya hivyo sasa wakati wakufurahi umefika,”mesema Chalamila.

Amesema mkandarasi anapaswa kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha barabara hiyo inakamilika ndani ya miezi 16  na mvua zikianza kunyesha   barabara iwe  inakaribia kukamilika ili wananchi wasipate usumbufu.

Ameeleza kuwa amepata taarifa kuwa kuna baadhi ya wakazi wa eneo hilo wameishtaki  Wakala wa Barabara Nchini (TANROAD),  hivyo  wataendelea kusikiliza maamuzi ya Mahakama na pindi hukumu ikitoka kama TANROAD imeshinda basi atachukua hatua za haraka kuhakikisha wanaboma nyumba zote zilizopo kwenye hifadhi ya barabara.

“Nimepata taarifa kuwa kuna baadhi ya wakazi wa hapa wameenda kuishtaki TANROAD jambo zuri sana ila niwahakikishie endapo hukumu itatoka TANROAD imeshinda sitachukua hata dakika 10 nitakuwa nimeshafika hapa na kijiko sitaangalia nini kimetoka au nani yupo ndani nitavunja zote,” amesema.

Chalamila amewataka wananchi kuchagua viongozi ambao wataendelea kuwaletea maendeleo na si kuwagawa na kuwacheleweshea maendeleo.

Vilevile ametoa rai kwa viongozi wa vyama vya siasa hasa CCM kuacha figisu wanazozifanya ndani ya chama na kusababisha kuchelewesha maendeleo kwa wananchi na pia vijana kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya  chama.

Naye Mbunge wa Jimbo la Segerea, Bona Kamoli amemshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuidhinisha pesa kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa barabara hiyo huku akitoa wito kwa serikali kuhakikisha wanakarabati mto Msimbazi kwani umekuwa ukiwafuata wananchi na si wananchi kufuata mto kama ilivyokuwa awali.

Amesema barabara ikikamilika itaongeza uchumi kwa wakazi wa maeneo hayo kwani watakuwa na uwezo wa kufanya kazi muda wote lakini hata watu wataongezeka kwani watakuwa na uhakika wa usafiri.

Ameongeza kuwa mchakato utakaoanza wa  mradi wa DMDP unatarajiwa kuanza Aprili,hivyo wanaomba mchakato huo usipelekwe mbele huku wakiomba Mungu mvua zisinyeenye kwa kipindi hiko ili barabara za mitaa zikamilike.

Naye Mbunge wa Jimbo la Ubungo, Profesa Kitila Mkumbo amesema ujenzi wa barabara hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya CCM kwani hiyo ilikuwa moja ya ahadi ya chama kwa wananchi wake.

Akizungumzia ujenzi wa barabara hiyo Mkurugenzi wa Barabara TANROAD, Mhandisi Jephason Nnko amesema ujenzi wa barabara hiyo utahusisha na ujenzi wa daraja la Kinyerezi, barabara ,  makalavati saba,  barabara ya watembea kwa mguu na kuwekwa kwa taa barabara yote ili kusaidia hata wafanyabiashara kuweza kufanyabiashara zao wakati wote.

Kwa upande wake Meneja Mradi wa Kampuni ya ujenzi, Nyanza Mhandisi Gilbert Bahesha amesema watahakikisha historia inaendelea kuandikwa katika barabara hiyo kwani wanatarajia kumaliza mradi huo kwa wakati uliopangwa ili kuendelea kukata kiu ya wananchi hao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles